

Lugha Nyingine
Jordan, Palestina, Misri zasisitiza kukataa mipango yoyote ya Israeli ya kuwaondoa Wapalestina kwenye maeneo yao (3)
AMMAN - Jordan, Misri na Palestina zimesisitiza Jumatano kwamba zinapinga mpango wowote wa Israeli wa kuwaondoa Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza kwenye mkutano wa kilele wa pande tatu uliofanyika mjini Aqaba, Jordan ambapo Mfalme Abdullah II wa Jordan, Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sisi, na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas pia wametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kulaani na kuchukua hatua dhidi ya mipango hiyo.
Wamesisitiza haja ya kuendelea kuishinikiza Israel kusimamisha uvamizi wake dhidi ya Gaza na kulinda raia wasio na hatia katika ukanda huo, kwa mujibu wa taarifa ya Kasri la Kifalme la Hashemite la Jordan.
Wakati huo huo, Rais Sisi wa Misri ametoa wito wa "msimamo wa wazi" kutoka kwa jumuiya ya kimataifa kushinikiza usimamishaji wa vita katika ukanda wa Gaza na kuelezea juhudi zinazofanywa na Misri kufungua mazungumzo na pande mbalimbali husika ili kufikia makubaliano ya mapatano huko Gaza.
Viongozi hao pia wameeleza kukataa kabisa majaribio yoyote ya kutaka kulimaliza suala la Palestina na kuitenganisha Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, sehemu ambazo zote ni sehemu muhimu za Taifa la Palestina, taarifa hiyo imeongeza.
Katika mkutano huo, viongozi hao watatu pia wamesisitiza umuhimu wa kuhakikisha misaada ya kibinadamu ya kutosha huko Gaza ili kupunguza hali mbaya ya kibinadamu katika eneo hilo.
Mfalme Abdullah II, Sisi na Abbas pia wameonyesha "kukataa kabisa majaribio yoyote ya kuikalia tena sehemu za Gaza," wakisisitiza ulazima wa "kuwezesha watu wa Ukanda wa Gaza kurejea makwao."
Kabla ya mkutano huo, mfalme wa Jordan alifanya mikutano tofauti ya pande mbili na marais wa Misri na Palestina kujadili juhudi za kusimamisha vita mara moja huko Gaza.
Mkutano huo wa Aqaba umefanyika huku waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken akiwa katika ziara ya Mashariki ya Kati kuhusu mgogoro wa Gaza. Hadi sasa ametembelea Uturuki, Ugiriki, Jordan, Qatar, Falme za Kiarabu, Saudi Arabia, Israel, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Bahrain, na anatarajiwa kuhitimisha safari yake kwa kuwasili mjini Cairo leo Alhamisi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma