

Lugha Nyingine
Benin yapokea dozi 215,900 za chanjo dhidi ya malaria
COTONOU - Serikali ya Benin imepokea dozi 215,900 za chanjo dhidi ya malaria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Cotonou siku ya Jumatatu na itaanza kuzitumia katika miezi ijayo.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Waziri wa Afya wa Benin Benjamin Hounkpatin amesema dozi za chanjo hiyo zimechukuliwa na serikali kwa msaada wa washirika wake katika sekta ya afya, wakiwemo Shirika la Afya Duniani, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, na Gavi, Muungano wa Chanjo, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea utoaji chanjo kwa wingi dhidi ugonjwa huo hatari zaidi kwa watoto wa Afrika.
"Kuingizwa kwa chanjo ya malaria katika Mpango wa Uliopanuliwa wa Utoaji Chanjo wa nchi hiyo ni hatua muhimu katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu nchini Benin," amesema waziri huyo na kuongeza kuwa utoaji wa chanjo hiyo ya malaria katika maeneo yaliyoathirika zaidi na ugonjwa huo unaweza kudhibiti ugonjwa huo na kuokoa makumi ya maelfu ya maisha kila mwaka.
“Mchanganyiko wa kupewa chanjo na hatua nyingine za kukabiliana na ugonjwa wa malaria, kama vile vyandarua vyenye viua wadudu, upuliziaji wa dawa kwa mabaki ya mbu ndani ya nyumba, tiba ya kinga ya mara kwa mara kwa wajawazito, na matumizi ya dawa za malaria, utasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vinavyotokana na malaria," amesema.
Malaria bado inaendelea kuwa janga kubwa la kudumu nchini Benin na ndiyo chanzo kikuu cha vifo miongoni mwa watoto chini ya miaka 5, ikichukua asilimia 40 ya wagonjwa wasio wa kulazwa hospitalini na asilimia 25 ya wanaolazwa hospitalini nchini humo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma