DRC yaanzisha operesheni za pamoja za kijeshi na ujumbe wa SADC dhidi ya waasi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 17, 2024
DRC yaanzisha operesheni za pamoja za kijeshi na ujumbe wa SADC dhidi ya waasi
Picha iliyopigwa Januari 16, 2024 ikimuonyesha Luteni Jenerali Fall Sikabwe, mratibu wa operesheni za kijeshi za Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wa Kivu Kaskazini, huko Goma, Mji Mkuu wa Jimbo la Kivu Kaskazini, Mashariki mwa DRC. (Picha na Alain Uyakani/Xinhua)

GOMA, DRC - Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) limetangaza Jumanne huko Goma, mji mkuu wa Jimbo la Kivu Kaskazini, kuanza kwa operesheni za pamoja za kijeshi dhidi ya waasi kwa kushirikiana na vikosi vya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo ambapo tangazo hilo limetolewa na Luteni Jenerali Fall Sikabwe, mratibu wa operesheni za kijeshi za Jeshi la DRC huko Kivu Kaskazini, wakati wa mkutano wa kwanza wa pamoja kati ya jeshi la DRC na SADC.

Kwa mujibu wa serikali ya DRC, kikosi hiki cha kijeshi cha SADC kitafanya operesheni za mashambulizi, haswa kulilenga kundi la waasi la Vuguvugu la Machi 23 (M23) ambalo linashikilia maeneo kadhaa katika eneo la Masisi na Rutshuru, katika Jimbo la Kivu Kaskazini.

"SADC inakuja na ujumbe wa mashambulizi. Kwa mamlaka ya wakuu wa nchi wanachama wa SADC, tutaanzisha operesheni kubwa dhidi ya maadui wa nchi yetu", amesema Fall Sikabwe na kusisitiza kuwa analazimika kukomesha uasi ambao umedumu kwa miezi kadhaa.

Kikiwa kinaundwa hasa na wanajeshi kutoka Afrika Kusini, Tanzania na Malawi, kikosi hiki cha kijeshi cha SADC kinachukua nafasi ya kikosi cha kikanda cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)ambacho serikali ya DRC inaona kuwa hakifanyi kazi na kukataa kuongeza muda wake.

Kwa sasa, ni Afrika Kusini na Malawi tu ambazo tayari zimepeleka baadhi ya wanajeshi wake huko Goma. Tanzania inatarajia kuhamisha wanajeshi wake na vifaa vyake ambavyo tayari viko nchini DRC ndani ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, ambao muda wake utamalizika mwishoni mwa 2024.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha