China yarusha chombo kipya cha kubeba mizigo kupeleka mahitaji kwenye kituo cha Tiangong cha anga ya juu cha China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 18, 2024
China yarusha chombo kipya cha kubeba mizigo kupeleka mahitaji kwenye kituo cha Tiangong cha anga ya juu cha China
Roketi ya Long March-7 Y8 iliyobeba chombo cha mizigo cha anga ya juu cha Tianzhou-7 ikiruka kutoka kwenye kituo cha urushaji vyombo kwenda anga ya juu cha Wenchang katika Mkoa wa Hainan, Kusini mwa China, Januari 17, 2024. (Xinhua/Liu Jinhai)

WENCHANG - Shirika la Anga ya Juu la China (CMSA) limesema, China imerusha chombo cha mizigo cha anga ya juu cha Tianzhou-7 Jumatano usiku ili kupeleka mahitaji muhimu kwa ajili ya kituo chake cha anga ya juu cha Tiangong kinachozunguka, ambapo roketi ya Long March-7 Y8, iliyokuwa imebeba chombo hicho, iliruka Saa 4:27 usiku (Kwa saa za Beijing) kutoka kituo cha urushaji vyombo kwenda anga ya juu cha Wenchang katika Mkoa wa Hainan, Kusini mwa China.

Baada ya dakika 10 hivi, chombo hicho cha Tianzhou-7 kilijitenga na roketi na kuingia kwenye obiti yake iliyopangwa kwenye anga ya juu. Paneli zake za jua zilijifungua punde baada ya hapo. Shirika hilo limetangaza urushaji huo kuwa na mafanikio kamili.

Urushaji huo wa siku ya Jumatano ni safari ya kwanza ya anga ya juu kwa mradi wa anga ya juu wa China mwaka huu. Pia ni safari ya 507 ya mfululizo wa roketi za kubeba mizigo za Long March.

Safari hiyo ni safari ya sita kwa mfumo wa uwasilishaji mahitaji kwenye kituo cha anga ya juu cha China unaojumuisha chombo cha kubeba mizigo cha Tianzhou na roketi ya kubeba mizigo ya Long March-7.

Chombo hicho kimebeba mahitaji mbalimbali vikiwemo vitu kama vile vya mfumo wa mwanaanga, mfumo wa kituo cha anga ya juu, mfumo wa matumizi, mfumo wa chombo cha kubeba mizigo kwenda anga ya juu. Pia kimebeba mahitaji muhimu ya wanaanga, ikiwa ni pamoja na bidhaa za Mwaka Mpya wa Jadi wa China, matunda na mboga mboga na vitu vingine ambavyo kwa ujumla vina uzito wa tani 5.6. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha