Madaktari wa China washiriki katika mapambano dhidi ya mlipuko wa kipindupindu nchini Zambia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 19, 2024
Madaktari wa China washiriki katika mapambano dhidi ya mlipuko wa kipindupindu nchini Zambia
Madaktari wa China wakifuatilia hali ya mgonjwa aliyeambukizwa kipindupindu katika Uwanja wa Taifa wa Mashujaa, uliotengwa maalum kuwa Kituo cha Matibabu ya Kipindupindu, mjini Lusaka, Zambia, Januari 18, 2024. (Xinhua/Peng Lijun)

LUSAKA - Madaktari wa China waliungana na wahudumu wa afya wa Zambia siku ya Alhamisi kutoa huduma za afya kwa wagonjwa wa kipindupindu huko Lusaka, mji mkuu wa Zambia ambapo madaktari jumla ya 10 kutoka Timu ya 24 ya Madaktari wa China na Timu ya 26 ya Madaktari Wataalam wa Jeshi la China walikuwa katika Uwanja wa Taifa wa Mashujaa, ambao umetengwa maalum kuwa kituo cha matibabu cha kitaifa, ili kutoa huduma kwa wagonjwa.

Du Xiaohui, Balozi wa China nchini Zambia, amesema kuwa timu hizo za madaktari zimeanza kazi katika kituo hicho cha matibabu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya viongozi wa nchi hizo mbili na hatua za msaada zilizotangazwa hivi karibuni na China.

Ubalozi wa China pia umetoa michango ya ziada kusaidia Zambia katika kukabiliana na mlipuko wa kipindupindu.

"Kwa mujibu wa mipango ya mamlaka ya afya ya Zambia, wataalamu hawa wa matibabu, watashirikiana na wenzao wa Zambia kutoa huduma za afya kwa wagonjwa," Du amesema kwenye hafla ya makabidhiano ya vifaa tiba.

Amesema wataalam wa matibabu wa China jumla ya 993 wamesafiri hadi Zambia katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita ili kukabiliana na magonjwa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na UVIKO-19, kipindupindu na malaria, akieleza dhamira ya China ya kuisaidia Zambia wakati wa mlipuko wa kipindupindu.

Waziri wa Afya wa Zambia Sylvia Masebo ameishukuru China kwa msaada wake huo, siyo tu katika sekta ya afya bali hata katika maeneo mengine. Amesisitiza urafiki wa kweli wa kindugu ulioonyeshwa na China, akisema kwamba viongozi wa sasa wa China umedumisha moyo wa viongozi wa zamani katika kudumisha uhusiano huo.

Waziri huyo pia ameshukuru michango hiyo akisema ni muhimu kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa kipindupindu ambao umeathiri nchi hiyo tangu Oktoba mwaka jana.

Zambia imerekodi visa 10,887 na vifo 432 kutokana na ugonjwa huo, huku kukiwa na juhudi zinazoendelea za kutibu wagonjwa katika vituo mbalimbali vya matibabu katika majimbo tisa.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha