

Lugha Nyingine
Felix Tshisekedi aapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa muhula mpya (2)
![]() |
Rais Mteule wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Felix Tshisekedi akishiriki kwenye sherehe za kuapishwa kwake huko Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Januari 20, 2024. (Str/Xinhua) |
KINSHASA - Felix Tshisekedi, Rais mteule wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ameapishwa siku ya Jumamosi kwenye hafla iliyofanyika kwenye Uwanja wa Mashujaa wa Kinshasa, na kuanza madaraka ya kipindi cha pili cha miaka mitano. Wakuu wa nchi wapatao 20, hasa kutoka Afrika, na wajumbe kadhaa wa ngazi za juu wa kigeni walishiriki kwenye hafla hiyo.
Mahakama ya Kikatiba ya DRC mapema Januari yalithibitisha rasmi kuchaguliwa tena kwa Rais Felix Tshisekedi kufuatia uchaguzi wa Desemba 20. Tshisekedi alipata asilimia 73.47 ya kura zote zilizopigwa, huku mgombea mkuu wa upinzani Moise Katumbi akiwa nyuma kwa asilimia 18.08.
Katika hotuba yake ya kuapishwa, Rais Felix Tshisekedi ameahidi kuchukua hatua, ikiwa ni pamoja na kuongeza nafasi za ajira, ulinzi wa uwezo wa manunuzi wa familia, usalama wa nchi, uendeshaji wa uchumi wa aina mbalimbali, na upatikanaji wa huduma za msingi. Alilaani tishio sugu dhidi ya DRC, huku akikaa kimya kwa muda wa dakika moja kuwakumbuka mashujaa waliofariki na waathiriwa waliouawa kwa ukatili nchini DRC.
"Leo, zama mpya zinazaliwa, ni zama za ukomavu, zama zilizotukuka, zama zilizopitishwa kwa kiapo kipya cha 'Usisaliti Kongo kamwe,'" Rais Felix Tshisekedi ametangaza.
Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi ya DRC iliyosimamia uchaguzi huo mkuu ilisema kuwa, raia wa DRC zaidi ya milioni 18 kati ya wapiga kura jumla ya milioni 44 waliojiandikisha, walipiga kura katika uchaguzi wa rais, Bunge la Taifa na mabaraza 26 ya majimbo. Hata hivyo, mchakato huo haukufanyika bila kuwa na utata kwani wagombea wa upinzani waliibua madai ya dosari, ambazo tume ya uchaguzi baadaye ilisema hazikuathiri matokeo ya uchaguzi.
Uchaguzi huo ulikuwa muhimu kwani ni wa pili kwa viongozi kukabidhiana madaraka kwa njia ya amani katika historia ya nchi hiyo tangu ipate uhuru Mwaka 1960. Mwaka 2018, Tshisekedi aliingia madarakani baada ya kushinda uchaguzi, ikiwa ni mara ya kwanza kwa viongozi kukabidhiana madaraka kwa amani nchini humo tangu nchi hiyo ipate uhuru kutoka kwa Ubelgiji.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma