

Lugha Nyingine
Bunge la Uturuki laidhinisha ombi la Sweden kujiunga na NATO (2)
ANKARA - Wabunge wa Uturuki wameidhinisha mswada uliocheleweshwa kwa muda mrefu juu ya azma ya Sweden kuwa nchi mwanachama wa 32 wa Jumuiya ya NATO siku ya Jumanne baada ya mjadala katika Bunge kuu la Taifa ambapo wabunge jumla ya 346 walishiriki katika upigaji kura, huku kura 287 zikiunga mkono, 55 zikipinga na wabunge wanne waliacha kupiga kura.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan anatarajiwa kutia saini mswada huo kuwa sheria ndani ya siku chache zijazo.
Kuidhinishwa huko kwa Bunge la Uturuki kumekaribishwa na Waziri Mkuu wa Sweden Ulf Kristersson. "Leo tuko hatua moja karibu kuwa mwanachama rasmi wa NATO," ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X, ambao zamani ulijulikana kwa jina la Twitter.
Kufuatia uidhinishaji huo wa Uturuki, Hungary inabaki kuwa nchi pekee mwanachama wa NATO ambayo haijaidhinisha ombi la Sweden kujiunga na jumuiya hiyo ya kijeshi.
Sweden na Finland zilituma maombi ya kujiunga na NATO baada ya Russia kuanzisha operesheni yake ya kijeshi nchini Ukraine Mwaka 2022.
Kujiunga kwao kunahitaji idhini ya pamoja ya nchi wanachama wote wa NATO.
Uturuki iliidhinisha ombi la NATO la Finland mwezi Machi mwaka jana lakini imekuwa ikienda polepole juu ya kujiunga kwa Sweden, ikitaka nchi hiyo ya Nordic kushughulikia zaidi masuala ya kiusalama yanayofuatiliwa na Ankara.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alitia saini itifaki ya Sweden kujiunga na NATO na kuiwasilisha bungeni mwezi Oktoba.
Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Uturuki iliidhinisha ombi la Sweden kujiunga NATO Desemba mwaka jana baada ya kujadiliwa, ikiwa ni hatua ya kwanza muhimu kuelekea kwenye upigaji kura kamili wa bunge.
Uturuki ilikuwa iko chini ya shinikizo kutoka Marekani kuidhinisha Sweden kujiunga na NATO, lakini Ankara imekuwa ikizuia uidhinishaji wake ili kuishinikiza Washington kuruhusu uuzaji wa ndege za kivita za F-16 kwa nchi hiyo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma