

Lugha Nyingine
Mradi wa usambazaji maji uliojengwa na kampuni ya China wanufaisha Watanzania 400,000
ARUSHA, Tanzania - Anna Emmanuel, mama wa watoto wanne anayeishi Njiro katika Jiji la Arusha, Kaskazini mwa Tanzania, hapitii tena tatizo la kukosa usingizi usiku akihofia kupata maji kwa ajili ya mahitaji ya nyumbani ambapo mama huyo wa nyumbani mwenye umri wa miaka 32 sasa anapata huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yake, kutokana na kampuni ya Ujenzi wa Nishati ya umeme ya China (PowerChina) kujenga mradi wa mfumo mpya wa usambazaji maji wa Arusha chini ya Mlima Meru.
Yeye ni miongoni mwa wanufaika 400,000 wa mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika, uliopangwa kukamilika Juni 27, 2023, kufuatia kuwekwa kwa jiwe lake la msingi Desemba 2018.
"Kabla ya mradi huo wa usambazaji maji kutekelezwa tulikuwa tukisafiri mbali kutafuta maji ya chemchemi ambayo mara nyingi hayakufaa kwa kunywa, kupika chakula na kufua nguo," Anna ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua katika mahojiano ya hivi karibuni. Amebainisha kuwa badala yake walilazimika kununua maji na mara nyingi watu hawaweza kumudu kutokana na matatizo ya kifedha waliyokumbana nayo.
Akiwa na tabasamu, Anna amesema, tangu kukamilika kwa mradi huo, sasa wanapata maji kwa ajili ya mahitaji ya kaya, na wanaweza kuokoa fedha kidogo walizonazo kwani hawana haja tena ya kununua maji.
"Siyo tu kwamba siku hizi tunapata maji safi na salama, lakini pia hatuna magonjwa yatokanayo na maji ambayo tuliyapata kutokana na maji machafu ya chemchemi," amesema.
Mradi huo wa usambazaji maji unajumuisha kutandaza mabomba ya chuma yenye urefu wa kilomita zaidi ya 620, kujenga mabwawa 11 na kuunganisha mtandao wa bomba la maji kwa kaya 48,000, kwa mujibu wa PowerChina.
Msimamizi wa mradi huo, Jin Denghui, amesema mradi huo unahusisha kuchimba maji kutoka kwenye kina kirefu chini ya ardhi katika mwanzo wa Mlima Kilimanjaro, mlima mrefu zaidi barani Afrika ulioko umbali wa kilomita 100 kutoka Arusha, na kuyasambaza kwa kaya lengwa jijini Arusha kila siku.
Wizara ya Maji ya Tanzania ilituma barua Januari mwaka 2022 kuwasilisha rasmi shukrani zake kwa PowerChina kwa mchango mkubwa wa kampuni hiyo katika kukamilisha mradi huo wa maji wa Arusha.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma