Hukumu ya rufaa ya Assange kupinga kurejeshwa nchini Marekani kutangazwa baadaye

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 22, 2024
Hukumu ya rufaa ya Assange kupinga kurejeshwa nchini Marekani kutangazwa baadaye
Bango linaloonyesha uungaji mkono kwa mwanzilishi wa WikiLeaks, Julian Assange likionekana kwenye maandamano nje ya Mahakama Kuu ya Uingereza mjini London, Uingereza, Februari 21, 2024. (Xinhua/Li Ying)

LONDON - Mahakama Kuu ya Uingereza siku ya Jumatano imehitimisha kusikiliza rufaa ya mwanzilishi wa WikiLeaks, Julian Assange ya kupinga kurejeshwa kwake nchini Marekani kwa tuhuma za ujasusi, lakini majaji wamesema watatoa uamuzi wao hapo baadaye.

Assange mwenye umri wa miaka 52, anatafutwa nchini Marekani kwa madai ya kufichua habari za ulinzi wa taifa kufuatia WikiLeaks kuchapisha mamia kwa maelfu ya nyaraka za kijeshi zilizovuja zinazohusiana na vita vya Afghanistan na Iraq muongo mmoja uliopita, ambazo zilijumuisha video ya helikopta ya Apache iliyorekodi jeshi la Marekani kuwapiga risasi waandishi wa habari wa Shirika la Habari la Reuters na watoto katika mitaa ya Baghdad Mwaka 2007.

Assange amekuwa akizuiliwa katika Gereza lenye ulinzi mkali la Belmarsh lililoko kusini mashariki mwa London tangu 2019. Mawakili wa Marekani walisema mapema kwamba ataruhusiwa kuhamia Australia, nchi yake ya asili, kutumikia kifungo chochote atakachopewa.

Uingereza iliidhinisha kurejeshwa kwake Marekani Mwaka 2022 chini ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo Priti Patel baada ya jaji hapo awali kuzuia uamuzi huo kwa hoja za hali ya afya ya akili ya Assange.

Assange hakuwepo kwenye kesi hiyo ya siku mbili kutokana na kuugua huku majaji wawili katika Mahakama Kuu ya Uingereza, ambao ni Victoria Sharp na Justice Johnson, wakisikiliza hoja kutoka kwa timu yake ya mawakili na wanasheria wanaoiwakilisha serikali ya Marekani.

Iwapo majaji hao wawili katika Mahakama Kuu ya Uingereza watatoa hukumu ya kumpendelea Assange, kesi kamili ya rufaa yake itapangwa kuzingatia pingamizi lake na inaweza kusababisha uamuzi mpya kuhusu kurejeshwa kwake.

Iwapo atashindwa katika kesi hiyo, Assange anaweza kurejeshwa nchini Marekani ndani ya wiki chache isipokuwa kama timu yake ya wanasheria inaweza kupata amri ya dharura katika Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu kwa wakati.

Mamia ya wafuasi wa Assange waliandamana nje ya Mahakama Kuu katikati mwa London Jumatano licha ya mvua kunyesha, wakiwa na mabango yaliyosomeka "Free Julian Assange" (Asange aachiwe huru) na wakipiga kelele za "Free Julian!" (Julian aachiwe) na "No extradition!" (Kutorejeshwa Marekani)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha