Timu ya madaktari wa China yahudumia wagonjwa zaidi ya 20,000 wa Sierra Leone wakati wa kazi yao ya mwaka mmoja

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 26, 2024
Timu ya madaktari wa China yahudumia wagonjwa zaidi ya 20,000 wa Sierra Leone wakati wa kazi yao ya mwaka mmoja
Daktari wa China akiongea na mgonjwa mwenyeji katika Hospitali ya Urafiki wa Sierra Leone na China huko Jui, mji mdogo ulio katika kitongoji cha Mji wa Freetown, Sierra Leone, Februari 22, 2024.(Xinhua/Xu Zheng)

FREETOWN - Kundi la 24 la timu ya madaktari wa China nchini Sierra Leone imetoa huduma kwa wagonjwa wenyeji zaidi ya 20,000 wakati wa kazi yake ya kipindi cha mwaka mmoja.

Chen Yongjun, kiongozi wa timu hiyo, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua katika mahojiano siku ya Alhamisi kwamba timu hiyo imefanya upasuaji zaidi ya 400 na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wengi wa tiba katika kipindi hicho.

Timu hiyo, ambayo ina wataalam 21 wa kiwango cha juu cha matibabu nchini China kutoka Mkoa wa Hunan, wanaotoa matibabu ya aina mbalimbali ya magonjwa ya mfumo wa neva na uzazi, na imepangwa kukamilisha kazi yake mwezi Machi baada ya timu nyingine kuwasili.

Akiielezea kazi hiyo kuwa yenye "changamoto," Chen amesema Hospitali ya Urafiki wa Sierra Leone na China, ambako timu hiyo inafanya kazi yake kwa muda mwingi, imekuwa ikikabiliwa na ukosefu wa umeme, maji na vifaa tiba, tatizo gumu linalopatikana katika hospitali nyingine nyingi nchini kote.

"Licha ya changamoto zote, tumekamilisha kazi yetu na kupata heshima kutoka kwa wataalam wenzetu na wagonjwa wa Sierra Leone," Chen amesema.

Melrose During, muuguzi mkuu wa uzazi wa hospitali hiyo, ameliambia Xinhua kwamba madaktari wa China daima wako tayari kuwafikia na kuwasaidia wenyeji.

"Wagonjwa wanawaamini na kujisikia vizuri wanapoingia. Ninapokuwa na mgonjwa mwenye tatizo gumu, huwapigia simu, na nimejifunza mengi," amesema During.

China ilituma timu yake ya kwanza ya madaktari nchini Sierra Leone Mwaka 1973 na tangu wakati huo imetuma jumla ya timu 24, na kutoa mchango katika kuboresha sekta ya afya ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Desemba Mwaka 2023, Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio aliandika kwenye ukurasa wake rasmi wa Mtandao wa X, ambao zamani ulifahamika kwa jina la Twitter, akisema, "Nimetoa shukrani zetu za dhati kwa timu ya madaktari wa China kwa juhudi zao za kuboresha utoaji wa huduma za afya wa nchi."

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha