Karakana ya Luban yasifiwa kwa kukuza ujuzi wa ufundi stadi wa wanafunzi nchini Ethiopia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 04, 2024
Karakana ya Luban yasifiwa kwa kukuza ujuzi wa ufundi stadi wa wanafunzi nchini Ethiopia
Yonas Akele akionyesha picha yake akiwa anashiriki kwenye hafla ya kuhitimu alipokuwa akisoma nchini China, katika Taasisi ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi ya Ethiopia mjini Addis Ababa, Ethiopia, Februari 15, 2024. (Xinhua/Li Yahui)

ADDIS ABABA - Ndani ya Karakana ya Luban huko Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, Yonas Akele, mwalimu wa Ethiopia mwenye umri wa miaka 39, anaelezea kwa wanafunzi uendeshaji wa mstari wa uzalishaji kiwandani kwa kutumia jukwaa la udhibiti wa kiotomesheni kutoka China.

Akele, kwa sasa ni mwalimu wa Taasisi ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi ya Ethiopia (FDRE), anajishughulisha na mpango wa mafunzo ya Karakana ya Luban. Mpango huu unaunganisha maarifa ya kinadharia na matumizi ya vitendo, kuwapa wanafunzi fursa ya kipekee ya kubadilisha ujuzi wanaojifunza darasani kuwa ustadi halisi.

Karakana ya Luban nchini Ethiopia, ambayo ni juhudi shirikishi kati ya FDRE na Chuo Kikuu cha Teknolojia na Elimu cha Tianjin cha China, ilizinduliwa Mwaka 2021.

Ikitoa kozi maalumu katika teknolojia ya roboti za viwandani, teknolojia ya mekatroniki, teknolojia ya udhibiti wa viwanda, na teknolojia ya kuhisi ya viwandani, karakana hiyo inalenga kuharakisha ukuzaji wa watu wenye ujuzi wa teknolojia ya kisasa ya viwanda vinavyohitajika sana katika mazingira yanayokua kwa kasi ya viwanda ya Ethiopia.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, karakana zaidi ya kumi na mbili chini ya jina la Lu Ban, ambaye alikuwa fundi katika China ya kale, zimeibuka katika bara zima la Afrika. Huku zikitoa elimu ya ufundi ya hali ya juu kwa vijana wa Afrika, karakana hizi zinaashiria kipengele muhimu cha ushirikiano wa China na Afrika katika kuwaandaa watu wenye ujuzi.

"Vijana nchini Ethiopia wana bahati ya kusoma hapa, na ninatarajia karakana zaidi za Luban zitaanzishwa nchini Ethiopia katika siku zijazo," Akele amesema.

Kwa ushirikiano na washirika kama vile makao makuu ya Umoja wa Afrika, Karakana ya Luban ya Ethiopia inapanua mchango wake nje ya mipaka ya Ethiopia.

Kupitia Mradi wa Ujuzi wa Afrika Mashariki kwa ajili ya Mageuzi na Ushirikiano wa Kikanda (EASTRIP), mpango wa pamoja wa Benki ya Dunia na serikali za Afrika kuboresha ubora wa programu za elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (TVET), karakana hii imeandaa vipindi vitano vya mafunzo hadi sasa, vikinufaisha vipaji vya vijana takriban 200 vya TVET kutoka Ethiopia, Kenya, Tanzania, na nchi nyingine.

"Karakana hii siyo tu imejitolea kukuza nguvu zetu za ndani na uwezo wa viwanda lakini pia inatumika kama kitovu cha kujenga uwezo katika eneo la Afrika Mashariki," amesema Haftom Gebregziabher, naibu mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi ya FDRE.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Deng Jie)

Picha