Ethiopia yazindua huduma ya data za satelaiti kwa ushirikiano na China (3)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 07, 2024
Ethiopia yazindua huduma ya data za satelaiti kwa ushirikiano na China
Melaku Muka, mkurugenzi wa operesheni za satelaiti katika Taasisi ya Sayansi ya Anga ya Juu na Data za Kijiografia ya Ethiopia (SSGI), akizungumza katika mahojiano na Shirika la Habari la China, Xinhua Machi 1, 2024, huko Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia. (Xinhua/Liu Fangqiang)

ADDIS ABABA - Taasisi ya Sayansi ya Anga ya Juu na Data za Kijiografia ya Ethiopia (SSGI) imezindua mpango wa "Kituo cha Ardhini kama Huduma", unaohusisha upokeaji wa data za satelaiti kwa nchi, mashirika na watumiaji mbalimbali, Melaku Muka, mkurugenzi wa operesheni za satelaiti katika SSGI amesema.

Amesema taasisi hiyo imeanza kujipatia mapato kwa kupokea data za satelaiti, kuzichakata na kuzichambua kwa ajili ya mashirika na nchi mbalimbali. Kituo cha ardhini kilichojengwa na China kwenye Kituo cha Uchunguzi na Utafiti wa Sayansi ya Anga ya Juu cha Entoto huko Addis Ababa ndicho kiini cha mpango huu, kikiwa na uwezo wa kupokea data za ubora wa juu za satelaiti.

"Taasisi imeanza kutoa huduma kamili za kituo cha ardhini, ikiwa ni pamoja na mawasiliano ya satelaiti, kupokea na kuchakata data, na kuwasilisha data hizo kwa wateja," Muka amesema katika mahojiano na Shirika la Habari la China, Xinhua huko Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia.

Kuzinduliwa kwa mpango huo kunaashiria hatua za Ethiopia za kujiunga na soko la kimataifa la data za satelaiti na kusaidia nchi hiyo ya Afrika Mashariki kupata mapato kutoka kwenye sekta hiyo.

Njia ya malipo ya huduma hiyo inapangwa kwa mujibu wa muda unaotumika kwenye kivukoau dakika inayotumiwa na kituo cha kupokea data. Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, mashirika ambayo hayana vituo vya msingi kwa sababu ya upungufu wa bajeti, waendeshaji satelaiti ambao wanahitaji mawasiliano na upokeaji wa data ya mara kwa mara, na taasisi za utafiti zinachukua huduma ya taasisi ya "Kituo cha Ardhini kama Huduma".

"Badala ya kujenga vituo vyao vyenyewe vya ardhini, watumiaji wanaweza kupata huduma za kituo hicho cha data cha gharama nafuu kwa kulipia tu kwa mujibu wa muda wanazotumia," mkurugenzi huyo amesema, akionyesha kuwa mpangilio huo unazifanya data za satelaiti za kimataifa kupatikana bila kutumia gharama kubwa.

Desemba 2019, Ethiopia ilirusha satelaiti yake ya kwanza ETRSS-1 kwenye anga ya juu kutoka China. Kituo cha maelekezo na udhibiti kiko kwenye kilima chenye urefu wa mita 3,200 cha Entoto, eneo la milimani nje kidogo ya Addis Ababa.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Deng Jie)

Picha