Bandari ya Dalian yaanza tena shughuli za usafiri wa meli za kimataifa za kitalii

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 11, 2024
Bandari ya Dalian yaanza tena shughuli za usafiri wa meli za kimataifa za kitalii
Watalii wanaosafiri kwa meli ya kitalii ya Zuiderdam wakiwasili kwenye Bandari ya Dalian, Mkoa wa Liaoning, Kaskazini Mashariki mwa China, Machi 10, 2024. (Xinhua/Pan Yulong)

DALIAN - Siku ya Jumapili, meli ya kitalii ya Zuiderdam inayoendeshwa na Kampuni ya Holland America Line ilitia nanga katika bandari ya Dalian, Mkoa wa Liaoning, Kaskazini-Mashariki mwa China, ikiashiria kuanza kwa shughuli za usafiri wa meli za kimataifa za kitalii katika Bandari hiyo.

Hii ni meli ya kwanza ya kimataifa ya kitalii kutembelea kaskazini mashariki mwa China tangu nchi hiyo itangaze kurejesha kikamilifu usafiri wa meli za kimataifa za kitalii kwenda na kutoka bandari zake Mwezi Septemba, 2023. Sasa miaka minne imepita tangu meli ya mwisho ya kimataifa ya kitalii kupokelewa na Dalian, mamlaka za mji huo zimesema.

Siku ya Jumapili asubuhi, watalii zaidi ya 2,000 na wafanyakazi wanaosafiri na meli hiyo, kutoka nchi na maeneo 47, walifika kwenye bandari hiyo ya Dalian kutoka Shanghai. Watalii hao wakiwa Dalian watatembelea maeneo mengi yenye mandhari nzuri mjini humo, huku pia walikuwa wamepanga kushiriki katika shughuli za kitamaduni.

Meli hiyo ya kitalii imepangwa kufika Tianjin kaskazini mwa China leo Jumatatu, huku ikiendelea na safari zake duniani kote.

Mji wa Dalian katika Mkoa wa Liaoning ni miongoni mwa miji ya kwanza kabisa ya China kuzindua shughuli za usafiri wa meli za kimataifa za kitalii.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Deng Jie)

Picha