Treni ya mwendo kasi ya Jakarta-Bandung yawa njia  mpya inayopendwa na Waindonesia wakati wa safari za Sikukuu ya Eid

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 02, 2024
Treni ya mwendo kasi ya Jakarta-Bandung yawa njia  mpya inayopendwa na Waindonesia wakati wa safari za Sikukuu ya Eid
Abiria wakiingia kwenye ukumbi wa kusubiria treni katika Stesheni ya Reli ya Halim huko Jakarta, Indonesia, Machi 17, 2024. (Xinhua/Xu Qin)

JAKARTA - Zahra Zalfa Farida, mfanyakazi mwenye umri wa miaka 26 mjini Jakarta, atakuwa anasafiri kwa mara yake ya sita kwa treni ya mwendo kasi ya Jakarta-Bandung, inayoitwa Whoosh, kurudi katika mji wake alikozaliwa katika Jimbo la Java Magharibi, Indonesia.

Tangu treni ya mwendo kasi ya Jakarta-Bandung izinduliwe kwa mara ya kwanza nchini Indonesia Oktoba 2023, Farida amekuwa akipanda treni hiyo karibu kila mwezi kurejea nyumbani.

Treni hiyo sasa imekuwa njia anayopendwa zaidi ya usafiri. Treni hiyo imerahisisha maisha yake, si tu kwa sababu Stesheni ya Halim iko karibu na nyumba yake, lakini pia kwa sababu treni yenyewe inaweza kumpeleka Bandung kwa kasi, ikitumia dakika 40 tu, ikilinganishwa na usafiri wa basi kwa saa mbili aliokuwa akitumia.

"Treni ya mwendo kasi inafanya kila kitu kuwa na ufanisi zaidi kwangu, kutoka eneo hadi wakati. Treni pia ni yenye starehe, safi sana na haina kelele za kusumbua. Hii inathamani bei yake," Farida ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua Jumapili.

Farida atapanda treni hiyo tena kwa ajili ya safari yake ya kwenda nje ya Bandung Aprili 8 kusherehekea siku ya Eid al-Fitr pamoja na familia yake inayotarajiwa kuangukia Aprili 10. Alikata tikiti wiki kadhaa zilizopita.

Eid ni mwisho wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani wa kuanzia alfajiri hadi machweo. Nchini Indonesia, nchi yenye Waislamu wengi zaidi, sikukuu hiyo ya Eid imehusishwa na utamaduni wa watu kurudi nyumbani, unaojulikana kama mudik, kujumuika na familia na jamaa.

Serikali ya Indonesia imekadiria kuwa watu angalau milioni 193 watasafiri kwenda katika miji yao wakati wa msimu wa usafiri wa watu wengi kwa ajili ya Eid. Idadi hiyo inajumuisha asilimia 71.7 ya watu wote nchini humo.

Huu utakuwa wakati wa kwanza wa Eid kwa treni ya mwendo kasi ya Jakarta-Bandung. Wizara ya Uchukuzi ya Indonesia inakadiria kuongezeka kwa idadi ya abiria wakati wa msimu wa wasafiri wengi, ambayo inaweza kufikia watu hadi milioni 1.42.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha