Watu 5 wauawa katika mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran nchini Syria, Iran yaapa kulipiza

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 02, 2024
Watu 5 wauawa katika mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran nchini Syria, Iran yaapa kulipiza
Waokoaji wakifanya kazi katika jengo lililobomolewa la ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus, Syria, Aprili 1, 2024. (Picha na Ammar Safarjalani/Xinhua)

DAMASCUS/TEHRAN – Watu takriban watano, akiwemo kamanda mkuu wa Iran, wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya jengo la ubalozi mdogo wa Iran katika mji mkuu wa Syria, Damascus siku ya Jumatatu ambapo Wizara ya Ulinzi ya Syria imesema shambulizi hilo lilitokea majira ya saa 11 jioni kwa saa za huko (1400 GMT) wakati Israel ilipofanya shambulizi kutoka eneo la milima ya Golan la Syria, ikilenga jengo la ubalozi huo mdogo.

Balozi wa Iran nchini Syria Hossein Akbari, akizungumza na waandishi wa habari mbele ya ubalozi wa Iran mjini Damascus baada ya shambulio hilo, amesema watu watano hadi saba wameuawa katika shambulio hilo.

Ameongeza kuwa ndege za kivita za Israel za F-35 zilirusha makombora sita kutoka kwenye eneo la milima ya Golan katika shambulio lengwa la “jinai” lililolenga jengo la ubalozi mdogo wa Iran.

Habari kutoka shirika la habari la Iran Tasnim zinasema, Mohammad-Reza Zahedi, kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) na naibu wake, Mohammad-Hadi Haji Rahimi, wameuawa katika shambulio hilo.

Wengine 12 wamejeruhiwa katika shambulio hilo, imeongeza habari hiyo.

Shirika la Uangalizi wa Haki za Binadamu la Syria linasema, mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya watu wanane, akiwemo kamanda wa ngazi za juu wa Kikosi cha Quds nchini Syria na Lebanon, pamoja na washauri wawili wa Iran na askari watano wa IRGC.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Faisal Mekdad, ambaye alifika katika eneo la tukio kufuatia shambulizi hilo, amelaani shambulio hilo na kusisitiza kuwa hatua hiyo haitaathiri uhusiano kati ya Syria na Iran.

Baadaye, katika mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa Iran Hossein Amir-Abdollahian, Mekdad alilaani vikali mashambulizi hayo ya "kihalifu" ya Israeli na kuyaita "ukiukwaji wa wazi" wa sheria za kimataifa, haswa Mkataba wa Vienna wa Uhusiano wa Kidiplomasia wa 1961, ambao unafafanua mfumo wa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi huru.

Amir-Abdollahian kwa upande wake amesema shambulio hilo limekiuka wajibu na mikataba yote ya kimataifa akisisitiza kuwa Israel itawajibika kwa matokeo ya hatua hiyo.

Tukio hilo linaashiria kuongezeka kwa kiasi kikubwa kwa uhasama kati ya Israel na Iran, kwa kuwa ni shambulio la kwanza kuathiri ubalozi wa Iran nchini Syria tangu kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria Mwaka 2011.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha