China na Tanzania zawakumbuka wataalam wa China waliofariki wakati wa ujenzi wa reli ya TAZARA

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 03, 2024
China na Tanzania zawakumbuka wataalam wa China waliofariki wakati wa ujenzi wa reli ya TAZARA
Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania Makame Mbarawa akizungumza kwenye hafla ya kukumbuka wataalamu wa China waliofariki dunia wakati wa ujenzi wa reli ya TAZARA jijini Dar es Salaam, Tanzania, Aprili 2, 2024. (Xinhua/Herman Emmanuel)

DAR ES SALAAM - Wafanyakazi wa ubalozi wa China, wawakilishi wa kampuni na jamii ya Wachina nchini Tanzania, na maofisa wa serikali ya Tanzania siku ya Jumanne wametoa heshima kwa wataalamu wa China waliofariki wakati wa ujenzi wa reli ya TAZARA miaka ya 1970.

Balozi wa China nchini Tanzania Chen Mingjian na Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania Makame Mbarawa walishiriki kwenye shughuli hiyo, wakiweka mashada ya maua kwenye makaburi katika eneo la Gongo la Mboto nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Wahandisi, mafundi na wafanyakazi wa China zaidi ya 100 walifariki wakiwa kazini wakati wa ujenzi wa reli ya TAZARA, ambalo ni tukio la kihistoria lisilofutika ambalo ni mnara wa urafiki kati ya China na Tanzania, na pia kati ya China na Afrika.

"Ni mashujaa ambao wamejenga mnara wa urafiki kati ya China na Tanzania na China na Afrika. Watu wa China na Afrika watakumbuka majina yao daima, kadri wanavyokumbuka reli ya TAZARA," amesema Chen.

Chen amesema TAZARA unaonyesha kuheshimiana na usawa, uvumilivu na moyo wa kimataifa, akiongeza kuwa unajumuisha kiini cha uhusiano kati ya China na Afrika na matarajio ya pamoja ya watu wa China na Afrika.

"Tunawashukuru sana wataalam wa China waliojitolea maisha yao wakati wa ujenzi; watanzania hawatasahau mchango wao katika maendeleo ya uchumi," Mbarawa amesema.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha