Meli ya Kimataifa ya Kitalii iliyobeba watalii zaidi ya 1,800 yawasili Tianjin, China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 08, 2024
Meli ya Kimataifa ya Kitalii iliyobeba watalii zaidi ya 1,800 yawasili Tianjin, China
Watalii wa kigeni wakiomba vibali vya muda vya kuingia nchini China kwenye kituo cha ukaguzi wa mpaka cha Dongjiang mjini Tianjin, Kaskazini mwa China, tarehe 7 Aprili 2024. (Xinhua/Sun Fanyue)

TIANJIN - Meli ya utalii ya Serenade of the Seas imetia nanga kwenye Bandari ya Kimataifa ya Meli za Utalii ya Tianjin katika mji wa bandari wa Tianjin, Kaskazini mwa China siku ya Jumapili asubuhi, ikiwa na watalii zaidi ya 1,800 kutoka nchi na maeneo 50.

Safari ya kitalii ya siku 275 kwa meli hiyo, ambayo imesajiliwa katika nchi ya Visiwa vya Bahama na kuendeshwa na Kampni ya Royal Caribbean, ndiyo njia ndefu zaidi ya kuzunguka Dunia kwa sasa. Tianjin ni kituo chake pekee katika China Bara, kampuni hiyo inasema.

Meli hiyo itatia nanga Tianjin kwa siku mbili na usiku mmoja, ikiwa na wafanyakazi zaidi ya 800 na watalii zaidi ya 1,800. Wengi wa watalii hao wataenda kutalii katika miji ya Beijing na Tianjin.

"Tunafanya kazi na meli hiyo ya utalii na kampuni ya bandari ili kurahisisha taratibu za kuruhusu abiria kuingia na kuwapa muda zaidi wa kusafiri nchini China," amesema Bi Linlin, afisa wa ukaguzi wa uhamiaji wa mji huo, akiongeza kuwa kutokana na kufufuka kwa kasi kwa sekta ya utalii wa meli ya China, mahitaji kutoka kwa watalii wa kigeni kutembelea maeneo yenye mandhari nzuri ya China na maeneo ya kihistoria yanaongezeka.

Liu Zinan, mwenyekiti wa Kampuni ya Meli za Utalii za Royal Caribbean, Tawi la Asia amesema, "Siku zote tunazingatia soko la China, na tumezamiria kujenga thamani kwa wateja wa China, maendeleo ya kijamii na kiuchumi, pamoja na utalii wa ndani na nje. Tuna imani kubwa katika uchumi wa China."

Kampuni ya Kimataifa ya Royal Caribbean ilitangaza mpango wake mpya wa njia za meli za utalii nchini China mwezi Machi, huku kukiwa na meli mbili za utalii zilizopangwa kufika katika bandari za Shanghai, Tianjin na Hong Kong. Muda wa mpango wa meli hizo kusafiri unaanzia Februari 2025 hadi Aprili 2026.

Bandari ya Meli za Kimataifa za Utalii ya Tianjin imekaribisha meli 22 za utalii na kushuhudia watalii 68,000 hadi kufikia sasa mwaka huu, amesema Dong Zichen, naibu meneja mkuu wa kampuni inayoendesha bandari hiyo.

"Tuna matumaini makubwa kuhusu kuimarika kwa sekta ya utalii wa meli mjini Tianjin," Dong amesema, huku akiongeza kuwa bandari hiyo inakadiriwa kupokea meli 100 za utalii zikiwa na watalii kuingia na kutoka zaidi ya 300,000 mwaka huu.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha