Ubalozi mdogo mpya wa Iran wafunguliwa mjini Damascus, Syria baada ya shambulizi la Israel

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 09, 2024
Ubalozi mdogo mpya wa Iran wafunguliwa mjini Damascus, Syria baada ya shambulizi la Israel
Bendera ya Iran ikipandishwa kwenye ubalozi mdogo mpya wa Damascus, Syria, tarehe 8 Aprili 2024. I (Picha na Ammar Safarjalani/Xinhua)

DAMASCUS - Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amefungua jengo jipya la ubalozi mdogo katika mji mkuu wa Syria, Damascus siku ya Jumatatu, karibu na jengo la awali lililobomolewa katika shambuzi la kombora la Israel siku chache zilizopita ambapo amehudhuria hafla ya uzinduzi wa ubalozi huo mpya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Faisal Mekdad.

Amir-Abdollahian aliwasili Damascus Jumatatu alasiri kwa ziara yake ya kwanza nchini humo tangu shambulizi hilo Israel dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran Aprili 1. Shambulizi hilo liliwaua viongozi waandamizi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), akiwemo Mohammad Reza Zahedi, kamanda mkongwe aliyekuwa akiongoza tawi la operesheni za kigeni la IRGC, Kikosi cha Quds, nchini Syria na Lebanon.

Kwenye ziara yake hiyo mjini Damascus, Amir-Abdollahian amekutana na Rais wa Syria Bashar al-Assad, Waziri wa Mambo ya Nje Faisal Mekdad, na maafisa wa Usalama wa Taifa wa Syria.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari pamoja na mwenzake wa Syria, Amir-Abdollahian amesisitiza tena kwamba Israel itapata "ulipizaji unaohitajika" kutokana na shambulizi lake hilo, huku pia akiilaumu Marekani kwa tukio hilo.

Amesema Marekani kutolaani shambulizi hilo la Israel dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus kunaonesha kwamba "Marekani imeruhusu Israel kufanya uhalifu huu,", huku akibainisha kuwa shambulizi hilo "lilifanywa kwa kutumia ndege za kivita na makombora ya Marekani."

Aidha, waziri huyo amesisitiza kuwa shambulizi hilo la Israel "halitapita bila majibu."

Kwa upande wake, Mekdad amelaani shambulizi hilo la Israel dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran akisema limekiuka sheria za kimataifa na maadili yote ya binadamu.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha