

Lugha Nyingine
Rwanda yaeleza kusikitishwa kwake juu ya utata wa Marekani kuhusu waathirika wa mauaji ya kimbari ya Mwaka 1994
![]() |
Rais wa Rwanda Paul Kagame akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Kigali, Rwanda, Aprili 8, 2024. (Picha na Cyril Ndegeya/Xinhua) |
KIGALI - Rais Paul Kagame wa Rwanda ameeleza wasiwasi wake kubwa siku ya Jumatatu juu ya Marekani kutotambua mauaji ya kimbari ya Mwaka 1994 kuwa ni mauaji dhidi ya Watutsi, baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anthony Blinken kuchapisha ujumbe kuhusu kumbukumbu ya maauaji hayo ya kimbari kwenye mtandao wa X, Blinken alisema, "Tunaomboleza maelfu ya Watutsi, Wahutu, Watwa na wengine ambao maisha yao yalipotea katika siku 100 za ghasia zisizoelezeka."
Wanyarwanda wengi wamemkosoa Blinken kwa kutotambua haswa kwamba mauaji hayo ya kimbari yalilenga Watutsi.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Kigali, mji mkuu wa Rwanda, Jumatatu, Kagame amesisitiza kuwa suala hilo lilijadiliwa na Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton, ambaye aliongoza ujumbe katika hafla ya kumbukumbu ya miaka 30 tangu kutokea kwa mauaji hayo ya kimbari iliyofanyika Jumapili mjini Kigali.
Utata wa namna ya kubainisha mauaji hayo ya kimbari unatokana na madai kwamba Jeshi la Rwandese Patriotic Front (RPF), ambalo ni kundi la waasi lililosimamisha mauaji hayo ya kimbari, lilitekeleza mauaji ya kulipiza kisasi wakati na baada ya mauaji hayo. Kagame amekuwa akitupilia mbali tuhuma hizo.
Kagame amesema anaamini alifikia maelewano na serikali ya Marekani toka karibia Mwaka 2014 ili waepuke ukosoaji wowote kuhusu kumbukumbu hiyo ya mauaji ya kimbari.
"Kuna siku 365 kwa mwaka. Tupe siku hiyo, Aprili 7, kisha unaweza kuwa na siku 364, kutulaumu kila siku kwa kila kitu ambacho hupendi kwetu," Kagame amesema.
Katika hotuba yake ya kumbukumbu hiyo siku ya Jumapili, Kagame alisema Wanyarwanda kamwe hawataelewa ni kwa nini nchi mbalimbali zinaendelea kutokuwa na uelewa wa wazi kwa makusudi juu ya nani alilengwa katika mauaji hayo ya kimbari, na kuielezea kuwa ni aina fulani ya kukataa kutokea kwake na pia ni uhalifu. "Rwanda itapinga kila mara," aliongeza.
Rwanda siku ya Jumapili ilianza wiki ya maombolezo ya kitaifa na siku 100 za kumbukumbu ya miaka 30 tangu kutokea kwa mauaji ya kimbari ya Mwaka 1994 dhidi ya Watutsi, ambapo zaidi ya watu milioni 1 waliuawa, kwa mujibu wa serikali ya Rwanda.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma