Lugha Nyingine
Wasomi wa Sudan Kusini na China waahidi kufanya ushirikiano kwa ajili ya maendeleo ya pamoja (4)
Liu Hongwu, mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Masomo kuhusu Afrika ya Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang, akihutubia Baraza la tatu la Washauri Bingwa la Sudan Kusini na China mjini Juba, Sudan Kusini, Aprili 12, 2024. (Xinhua/Han Xu) |
JUBA - Wasomi wa Sudan Kusini, pamoja na wenzao wa China, siku ya Ijumaa katika Baraza la tatu la Washauri Bingwa la Sudan Kusini na China lililofanyika Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini wameahidi kuimarisha ushirikiano wao katika utafiti na kubadilishana maarifa ili kutoa mchango kwa ajili ya maendeleo ya nchi zao.
Pande hizo mbili zimebadilishana ujuzi na uzoefu kuhusu masuala mbalimbali muhimu katika ushirikiano wa nchi hizo mbili katika baraza hilo.
Robert Mayom Deng, makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Juba amesema, nchi hizo mbili zinahitaji kuimarisha ushirikiano wao katika sekta ya elimu, huku akiongeza kuwa juhudi hizi zitasaidia nchi zote mbili kujenga mfumo wa kubadilishana maarifa ambao unaweza kuongeza uwezo kwa maendeleo endelevu na kuimarisha ushirikiano wao kwa maendeleo ya pamoja.
Baraza hilo lililofanyika chini ya kaulimbiu ya "kuimarisha ushirikiano kwa maendeleo ya pamoja," lilianzishwa kwa pamoja na Taasisi ya Masomo ya Mikakati na Sera yenye makao yake makuu mjini Juba na Taasisi ya Masomo kuhusu Afrika ya Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang. Baraza la kwanza lilifanyika Juba Mwaka 2019, na la pili likifanyika mwezi Desemba 2021.
Deng amesema, China ni muhimu katika kuleta amani na utulivu nchini Sudan Kusini. "Ikiwa moja ya nchi kubwa duniani, ninaamini China inaweza kufanya hivyo. Utulivu huu unaweza kuendeleza maendeleo ya nchi yetu kwa sababu tukiwa na maendeleo haya endelevu, basi yataathiri watu wetu kwa njia chanya zaidi. China inaweza kufanya hivyo kwa kuchangia ujuzi na uzoefu wake katika ujenzi wa uwezo,” ameongeza.
Lin Chen, katibu mkuu wa Kituo cha Taaluma kuhusu Sudan Kusini cha Taasisi ya Masomo ya Afrika katika Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang na mchambuzi wa mradi katika Shirika la Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP), amesema "kituo hicho kimekuwa na umuhimu katika kuendeleza mazungumzo ya kitaaluma, kuhimiza maelewano na kutoa mchango katika maendeleo na ustawi wa ushirikiano kati ya China na Sudan Kusini. Ingawa tunajivunia mafanikio haya, tunafahamu kwa kutosha kwamba bado kuna kazi kubwa zaidi ya kufanywa.
Ma Qiang, Balozi wa China nchini Sudan Kusini amesema kuwa Baraza hilo limekuwa na mchango chanya katika kuendeleza maendeleo ya jumla ya uhusiano wa pande mbili kwa kuimarisha uhusiano wa watu kwa njia ya mawasiliano na kujumuisha mawazo, kuongeza maelewano kwa kujifunza kutoka kwa kila upande na kufanya kazi kwa ajili ya maslahi makubwa zaidi ya nchi zote mbili.
Baraza la Washauri Bingwa la Sudan Kusini na China linalenga kuinua uwezo wa utafiti wa kitaaluma wa China na Sudan Kusini. Linatafuta namna ya kuwezesha mabadilishano ya uzoefu katika utafiti wa sera, maendeleo ya kijamii na kiuchumi, uhifadhi wa mazingira, na nyanja zingine.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma