Reli zilizojengwa na China zavutia Waethiopia kwa usafiri wa kijani na wa bei nafuu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 24, 2024
Reli zilizojengwa na China zavutia Waethiopia kwa usafiri wa kijani na wa bei nafuu
Picha iliyopigwa Septemba 20, 2015 ikionyesha treni ikiendeshwa kwenye reli nyepesi huko Addis Ababa, Ethiopia. (Xinhua/Sun Ruibo)

ADDIS ABABA - Kwa miaka 15 iliyopita, Natnael Nigussie amekuwa akifanya biashara ndogo ndogo, akiuza vipodozi na nguo za kike, katika eneo lenye shughuli nyingi liitwalo Legehar katikati mwa Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia.

Utaratibu wake wa kila siku ulikuwa ukianza kwa kuendesha gari kwa saa mbili kupitia pilika za safari za asubuhi zenye changamoto nyingi ili kufikia duka lake dogo kutoka nyumbani kwake katika kitongoji cha mashariki mwa mji huo.

Nigussie alichangamka kwa furaha alipoelezea ukombozi wake mpya kutoka kwenye jinamizi hilo la foleni za magari na manufaa ya kuokoa muda ya Treni ya Reli Nyepesi ya Addis Ababa (AALRT), ambayo ilianza kutumika mwaka 2015.

Mamia ya maelfu ya watu wanasafiri kwa reli hiyo nyepesi kila siku kutoka stesheni 39 kote mjini humo.

"Baada ya kuanza kusafiri kwenye reli hiyo, kwenda katikati mwa mji siyo jinamizi tena la foleni ya magari. Muda ndiyo jambo la msingi kabisa kwenye biashara yangu," amesema kijana huyo mwenye umri wa miaka 32 huku akitabasamu. "Shukrani kwa reli hiyo nyepesi, ninatumia chini ya nusu ya muda kusafiri hadi Legehar, ambapo duka langu lililopo. Imekuwa ni mabadiliko makubwa kwangu."

Ikiwa ilijengwa na Shirika la Uhandisi wa Reli la China, reli hiyo nyepesi yenye urefu wa kilomita 34 ilianza kufanya kazi mjini Addis Ababa Septemba 2015. Mji huo una wakazi wanaokadiriwa kufikia milioni 5 na pia ni makao makuu ya Umoja wa Afrika na Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika.

Binyam Beyene, ambaye pia ni mkazi wa Addis Ababa ambaye anasafiri kwa reli hiyo kila siku, amesifia sana reli hiyo nyepesi kwa huduma yake ya usafiri wenye ufanisi na wa gharama nafuu na mchango wake mkubwa katika kuwezesha usafiri wa kutoa kaboni chache nchini Ethiopia na vile vile kelele ya chini na viwango vyake vya chini vya uchafuzi wa hewa.

Reli hiyo nyepesi iliyojengwa na China ilisafirisha watu zaidi ya milioni 109 katika miezi 41 ya kwanza tangu ianze kufanya kazi, na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa foleni ya magari na uchafuzi wa mazingira katika mji wa Ethiopia, kwa mujibu wa Shirika la Uhandisi wa Reli la China.

Reli ya Ethiopia-Djibouti yenye urefu wa kilomita 752.7, ikiwa ni moja ya matokeo ya mapema ya ushirikiano kati ya Ethiopia na China chini ya Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja (BRI) lililotolewa na China, imepata sifa tele kutokana na mchango wake mkubwa kwa ajili ya maendeleo ya Ethiopia.

Takwimu kutoka kwa Kampuni ya Ubia ya Reli ya Ethiopia na Djibouti zinaonyesha kuwa reli hiyo iliingiza birr bilioni 2.84 (kama dola milioni 50 za Kimarekani) katika miezi tisa ya kwanza ya mwaka wa fedha wa Ethiopia 2023/2024, ulioanza Julai 8, 2023. Mapato yanayopatikana yameongezeka kwa takriban dola milioni 1.12 za Kimarekani ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.

Reli hiyo kuu inayotumia umeme ilisafirisha abiria 148,664 katika kipindi hicho, ikiwa ni ongezeko la asilimia 15 ikilinganishwa na mwaka jana wakati kama huo.

Costantinos Bt. Costantinos, profesa wa sera za umma katika Chuo Kikuu cha Addis Ababa nchini Ethiopia, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba wakati Ethiopia imekumbwa na migogoro na ukame, maendeleo yake ya kiuchumi na mtandao wake miundombinu umeshuhudia "mageuzi makubwa chini ya BRI na Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika."

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha