Kuongezeka kwa mzigo wa deni la umma, kupungua kwa nafasi ya mambo ya fedha kunaiacha Afrika njia panda: UNECA

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 24, 2024
Kuongezeka kwa mzigo wa deni la umma, kupungua kwa nafasi ya mambo ya fedha kunaiacha Afrika njia panda: UNECA
Watu wakihudhuria Mkutano wa 10 wa Baraza la Kanda ya Afrika kuhusu Maendeleo Endelevu mjini Addis Ababa, Ethiopia, tarehe 23 Aprili 2024. (Xinhua/Michael Tewelde)

ADDIS ABABA - Kuongezeka kwa mzigo wa deni la umma kutokana na majanga yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi na kupungua kwa nafasi ya mambo ya fedha kwa sababu ya kuongezeka kwa mahitaji ya kifedha kumeiweka Afrika njia panda, Claver Gatete, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika (UNECA) amesema.

Ameyasema hayo siku ya Jumanne kwenye ufunguzi wa mkutnao wa 10 wa Baraza la Kanda ya Afrika kuhusu Maendeleo Endelevu mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Kaulimbiu ya mkutano huo ni "Kuimarisha Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu na Ajenda 2063 na kutokomeza umaskini wakati wa majanga mbalimbali: utoaji wa suluhu zenye ufanisi, thabiti na bunifu."

Akisisitiza udharura wa kushughulikia changamoto muhimu zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi na changamoto za mambo ya fedha katika bara zima, Gatete amesema miundombinu ya Afrika na mahitaji ya mabadiliko ya tabianchi yanakadiriwa kugharimu kati ya dola bilioni 68 na 108 za Kimarekani kila mwaka.

"Ingawa hadhi ya Afrika ya kuwa nafasi ya pili kwa kuwa eneo lenye uchumi unaokua kwa kasi duniani imethibitisha nguvu yake ya ustahimilivu wa ajabu, hatuwezi kupuuza hali halisi ya umaskini, njaa na ukosefu wa usawa barani humo," katibu mkuu huyo amesema.

Akikumbuka kwamba viongozi wa Afrika hivi karibuni wameelezea wasiwasi wao kuhusu kukosa kwa mfumo wa fedha duniani ili kukidhi mahitaji yanayoendelea ya bara hilo, ametoa wito wa kuunda upya mfumo wa fedha duniani ili kutomuacha mtu nyuma.

Amesema Umoja wa Mataifa umebainisha maeneo sita ya njia kuu za uwekezaji katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), ambayo ni pamoja na kuboresha mifumo ya chakula, upatikanaji wa nishati na uwezo wa kumudu gharama zake, muunganisho wa kidijitali, elimu na uhifadhi wa kijamii.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha