Israel yazidisha mashambulizi huko Gaza, na kushambulia maeneo 120 (6)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 14, 2024
Israel yazidisha mashambulizi huko Gaza, na kushambulia maeneo 120
Moshi ukipaa angani kufuatia mashambulizi ya Israeli katika kambi ya wakimbizi ya Jabaliya, Kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, Mei 13, 2024. (Picha na Abdul Rahman Salama/Xinhua)

JERUSALEM - Jeshi la Israel limesema Jumatatu kuwa limezidisha mashambulizi yake kutoka kaskazini hadi kusini katika Ukanda wa Gaza, likilenga maeneo 120 katika mji wa Rafah, vitongoji vya Jabaliya na Zeitoun katika mji wa Gaza.

Kikosi cha kijeshi cha Israel cha 162 kilikuwa kikipigana mashariki mwa Rafah na upande wa Gaza wa kivuko cha Rafah, kikianzisha "mashambulizi dhidi ya maeneo lengwa ya Hamas," ikiwa ni pamoja na kurusha roketi, na kuua wanamgambo "kadhaa" katika mapigano ya ana kwa ana, jeshi la Israel limesema katika taarifa yake.

Jeshi hilo limesema linaendesha operesheni "ndogo" dhidi ya miundombinu ya wanamgambo huko Rafah, wakati Umoja wa Mataifa ukiripoti kuwa Wapalestina zaidi ya 300,000 wamekimbia Rafah tangu wikiendi iliyopita wakati wanajeshi wa Israeli wakisonga mbele zaidi katika mji huo.

Kikosi cha makomando na askari wa miguu wamevamia Jabaliya kutoka ardhini huku kikosi cha anga cha jeshi hilo kikifanya mashambulizi ya anga. Wanajeshi hao walikuwa wakishiriki katika "mapambano ya kukaribiana," jeshi hilo limesema, na kuongeza kuwa "miundombinu mingi ya chini ya ardhi na maeneo ya mapigano katika eneo hilo yameharibiwa."

"Katika moja ya mashambulizi, jengo la kijeshi limebomolewa ambapo kundi la magaidi wa Hamas walikuwa wamekusanyika," imesisitiza taarifa hiyo, na kuongeza kuwa mashambulizi ya ardhini na ya angani yamefanywa pia Zeitoun.

Jeshi limesema kuwa wanajeshi jumla ya 11 wamejeruhiwa katika Ukanda wa Gaza tangu Jumamosi. Miongoni mwao, askari watano na mfanyakazi wa ziada wa kiraia wa jeshi wamepata majeraha makubwa, wakati waliobaki wamepata majeraha kiasi.

Idadi ya vifo vya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza imeongezeka hadi 35,091, kwa mujibu wa mamlaka ya afya huko Gaza, ikiwa ni pamoja na watu 57 waliouawa na jeshi la Israel katika siku moja iliyopita.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha