

Lugha Nyingine
Watu 4 waokolewa, wengine bado wamenaswa baada ya jengo lililobomolewa kuporomoka nchini Kenya
NAIROBI - Watu wanne wameokolewa kutoka kwenye vifusi vya jengo la makazi lililoporomoka siku ya Jumanne katika eneo la Kiamaiko mjini Kenya Nairobi, Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Nairobi Adamson Bungei amesema, na kuongeza kuwa watatu kati yao wamepelekwa katika kituo cha afya kilicho karibu, huku mmoja aliyepata majeraha madogo amepata matibabu katika eneo la tukio, na kwamba shughuli ya kutafuta na kuokoa waathiriwa zaidi inaendelea.
Mashuhuda wamesema kuwa watu takriban 10 walikuwa wakitafuta vyuma chakavu katika jengo hilo lililokuwa limewekewa alama ya kubomolewa na maafisa wa serikali, lilipoporomoka bila kutarajiwa.
Wakaazi wa eneo hilo wamesema kuwa jengo hilo ni miongoni mwa majengo kadhaa yaliyowekewa alama ya kubomolewa kufuatia mafuriko makubwa ambayo yalisababisha uharibifu wa majengo karibu na mito, haswa katika makazi yasiyo rasmi.
Hali hiyo imesababisha maandamano katika eneo hilo, huku kukitolewa wito wa kupewa makazi mbadala kwa walioathirika.
Waziri wa Mambo ya Ndani na Utawala wa Serikali ya Kitaifa ya Kenya Kithure Kindiki amesema kwamba wale ambao wamevamia maeneo ya kanda ya mito na chemchemi lazima waondoke mara moja, akionya kwamba kama watakaidi amri hiyo watahamishwa kwa nguvu.
Mvua kubwa imekuwa ikinyesha katika maeneo kadhaa nchini humo tangu Machi, na kusababisha vifo vya watu 289. Serikali ya Kenya imetahadharisha kuhusu hatari ya mafuriko katika maeneo ya mabondeni, pembezoni mwa vyanzo vya maji na mijini, huku kukiwa na uwezekano wa kutokea kwa maporomoko ya ardhi katika maeneo yenye miteremko mikali, miinuko na makorongo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma