DRC yafanya mazishi ya waathirika wa milipuko mibaya ya makombora katika maeneo ya IDP

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 16, 2024
DRC yafanya mazishi ya waathirika wa milipuko mibaya ya makombora katika maeneo ya IDP
Msafara wa magari ukiwa njiani kuelekea kwenye mazishi huko Goma, Jimbo la Kivu Kaskazini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mei 15, 2024. (Picha na Zanem Nety Zaidi/Xinhua)

GOMA - Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imefanya mazishi siku ya Jumatano kwa waathirika wa milipuko ya hivi karibuni katika maeneo kadhaa ya wakimbizi wa ndani (IDPs) katika jimbo la mashariki la Kivu Kaskazini iliyotokea Mei 3, ambapo roketi angalau tano zilianguka ndani na karibu na kambi nne za IDP na kwa mujibu wa serikali ya jimbo hilo, idadi ya waliofariki imeongezeka hadi 35 na wengine 37 kujeruhiwa.

Waziri wa mambo ya jamii, vitendo vya ubinadamu na mshikamano wa kitaifa wa DRC, Modeste Mutinga Mutushayi, amesisitiza nia na dhamira ya serikali ya DRC ya kutoacha juhudi zozote za kurejesha amani katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

"Naomba maombolezo haya yaamshe hamasa ya mshikamano wetu wa kitaifa. Muwe na uhakika zaidi kwamba hamko peke yenu katika majaribu haya magumu na ya kusumbua," amesema.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Mambo ya Ubinadamu (OCHA) ilionya siku ya Jumanne wiki iliyopita kwamba hatari ya milipuko zaidi ya makombora "haiwezi kuelezwa kutokuwepo," kwani moja ya makombora yaliyoanguka bado hayajalipuka, na kuna kuongezeka kwa uhasama katika maeneo yanayozunguka kambi za IDP.

Maeneo yaliyolipuliwa kwa makombora Ijumaa iliyopita yapo kwenye mhimili kati ya Goma na mji wa Sake, moja ya vituo vya uhasama kati ya jeshi la DRC na waasi wa Vuguvugu la Machi 23 (M23), unachukuliwa kuwa kizuizi cha mwisho kwa Goma.

Ufikiaji wa msaada wa ubinadamu kwa maeneo ya IDP kwenye mhimili huo wa Goma-Sake "umezuiliwa zaidi" kutokana na mapigano yanayoendelea, OCHA imesema.

Serikali ya DRC imelaumu mashambulizi hayo kufanywa na Kundi la M23, ambalo limechukua udhibiti wa baadhi ya maeneo ya Jimbo la Kivu Kaskazini.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, unaojulikana kwa jina la MONUSCO, umetoa wito kwa pande zote kuchukua hatua zinazofaa ili kupunguza hatari kwa ulinzi wa raia na kudumisha ufikiaji wa msaada wa ubinadamu.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha