

Lugha Nyingine
Mjasiriamali wa Chongqing awapa watu wenye ulemavu wa kusikia uwezo wa kuwasiliana vyema na dunia
Tian Ye ni mfanyabiashara mwenye ulemavu wa kusikia, kampuni yake, Kampuni ya Teknolojia ya Chongqing Yuermeng, imeunda jukwaa la kubadilishana utamaduni na uzoefu kuhusu jamii yenye ulemavu wa kusikia, pamoja na kamusi ya lugha ya ishara.
Kampuni hiyo inatoa video 8,000 za kufundisha lugha ya ishara na imeanzisha mfumo wa mwongozo wa lugha ya ishara kwenye maeneo ya umma. Mfumo huu tayari unatumika katika majumba tisa ya makumbusho mjini Chongqing, na kunufaisha watu zaidi ya milioni 10.
Asilimia 90 ya wafanyakazi katika timu ya Tian, ambao wengi wao wamehitimu kutoka Chuo Kikuu cha Ualimu cha Chongqing (CNU), wana ulemavu wa kusikia. Wamejitolea kushughulikia changamoto za mawasiliano na upatikanaji wa habari zinazokabili jamii yenye ulemavu wa kusikia, na kuwapa msaada kwa habari rahisi.
Wakati wa kujenga mfumo huo wa mwongozo wa lugha ya ishara, Tian na wenzake walitoa kipaumbele changamoto zinazokabili jamii yenye ulemavu wa kusikia na mahitaji yao, ili kuhakikisha maelezo sahihi na yanayoeleweka kwa lugha ya ishara. Baada ya uchunguzi wa kina na maboresho, timu hiyo imefanikiwa kuunda mfumo wa mwongozo.
Kwa kutupia macho siku za baadaye, Tian analenga kushirikiana na majumba zaidi ya makumbusho na taasisi za umma kote nchini China ili kukidhi mahitaji ya habari ya watu wenye ulemavu.
"Watu wenye ulemavu wa kusikia wana uwezo wa ajabu wa kufanikiwa kwa chochote, isipokuwa kusikia," Tian amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma