

Lugha Nyingine
Waziri wa mambo ya nje wa China akutana na wageni wa nchi za nje
BEIJING - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, ambaye pia ni Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China, amekutana kwa nyakati tofauti na wageni wa nchi za nje waliokuja China kuhudhuria mkutano wa 10 wa mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na nchi za Kiarabu, mjini Beijing siku ya Jumatano.
Alipokutana na Abdul-Hamid Dbeibah, Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya, Wang amesema kuwa China siku zote inaiunga mkono Libya katika kufikia maendeleo tulivu, na kulinda mamlaka, uhuru na ukamilifu wa ardhi yake ya kitaifa. Amesema China inapenda kushirikiana na Libya ili kuzidisha hali ya kuaminiana ya kisiasa, kuongeza mawasiliano, na kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kirafiki kati ya pande hizo mbili.
Kwa upande wake Dbeibah amesema kuwa, Libya inatilia maanani sana kuendeleza uhusiano kati yake na China na inafuata kwa dhati kanuni ya kuwepo kwa China moja. Amesema, Libya inatarajia China kutoa mchango mkubwa zaidi katika kuendeleza suluhu ya mapema ya suala la Palestina.
Wang alipokutana na naibu waziri mkuu wa Iraq ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Fouad Hussein amesema China inaiunga mkono kithabiti Iraq katika kulinda mamlaka, usalama, umoja na ukamilifu wa ardhi ya taifa, inaunga mkono serikali ya Iraq katika kuendeleza uchumi, kuboresha maisha ya watu na kupambana na ugaidi, na kupinga uingiliaji wa nje katika masuala ya ndani ya Iraq.
Kwa upande wake Hussein amesema kuendeleza uhusiano kati yake na China ni kipaumbele cha mambo ya diplomasia ya serikali ya Iraq, na Iraq daima inaiunga mkono China katika kulinda maslahi yake makuu.
Kwenye mkutano na Ahmed Aboul Gheit, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Wang amesema kuwa Chinainapenda kushirikiana na nchi za Kiarabu, ikiongozwa na makubaliano muhimu yaliyofikiwa na wakuu wa China na nchi za Kiarabu, ili kuzidisha mawasiliano na ushirikiano katika nyanja mbalimbali.
Kwa upande wake Gheit amesema Nchi za Kiarabu zinapenda kushirikiana na China kufanya juhudi kwa pamoja ili kufungua mustakabali mpana zaidi wa uhusiano kati ya Nchi za Kiarabu na China. Nchi za Kiarabu daima zinafuata kithabiti kanuni ya kuwepo kwa China moja, ameongeza.
Wang pia alikutana na mawaziri wa mambo ya nje na wawakilishi kutoka nchi za Mauritania, Algeria, Syria na Morocco ambapo wamejadili masuala kuhusu maslahi ya pamoja na masuala ya kikanda na kimataifa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma