Kampuni ya kauri ya China yawezesha ujenzi wa makazi ya bei nafuu nchini Kenya

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 04, 2024
Kampuni ya kauri ya China yawezesha ujenzi wa makazi ya bei nafuu nchini Kenya
Mfanyakazi akiendesha mashine ya kubeba mizigo, Forklift kuhamisha vifurushi vya vigae kwenye kiwanda cha bidhaa za kauri cha KEDA (Kenya) katika Kaunti ya Kajiado, Kenya, Mei 17, 2024. (Xinhua/Li Yahui)

NAIROBI - Mchana wa siku moja, wafanyakazi wa kiwanda cha Kampuni ya kauri cha KEDA (Kenya), kilichoko umbali wa kilomita takriban 70 kusini mwa mji mkuu wa Kenya, Nairobi, walikuwa na shughuli nyingi za kufungasha vigae vya sakafu kwenye maboksi ya rangi mbalimbali ili kusafirishwa hadi maeneo ya wateja.

Likiwa lilianzishwa Mwaka 1992, Kundi la kampuni za Viwanda za KEDA, kampuni yenye makao yake makuu nchini China inayojishughulisha hasa na utengenezaji na uuzaji wa mashine za vifaa vya ujenzi, ilianzisha kiwanda cha kutengeneza kauri cha KEDA katika kaunti ya kusini ya Kajiado nchini Kenya, kwa ubia na Kampuni ya Guangzhou Sunda ya China Mwaka 2016.

Li Ruiqin, mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo nchini Kenya, amesema uwekezaji wao katika utengenezaji wa vigae vya ubora wa juu umekuwa mfano wa kufufua sekta ya viwanda nchini humo ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kutoa fursa za ajira.

Kwa mujibu wa Li, kuanzisha kiwanda hicho cha vigae vya kauri katika maeneo ya vijijini kumeleta manufaa kwa uchumi wa eneo hilo, akitolea mfano biashara za hoteli na usafirishaji ambazo zimeshamiri tangu kuanzishwa kwa kiwanda hicho.

"Wakati ambapo nyayo zetu katika soko la Kenya zinapanuka, KEDA imefuata sera na kanuni za nchini humo ukiachilia mbali kuwekeza katika miradi ya uwezeshaji wa jamii ikiwa ni pamoja na shule, barabara na usambazaji wa maji," amesema Li kwenye mahojiano na Shirika la Habari la China, Xinhua akiwa kiwandani hapo.

Li amebainisha kuwa KEDA imeanzisha viwanda viwili vya vigae vya kauri, kimoja katika Kaunti ya Kajiado na kingine katika Kaunti ya Kisumu, na kiwanda kingine cha kutengeneza vifaa vya usafi, vyote vinachukua eneo la ardhi lenye ukubwa wa ekari 300 (kama mita za mraba milioni 1.2).

Viwanda hivyo viwili vya vigae vya kauri vina uwezo wa kuzalisha vigae vya sakafu vya mita za mraba 110,000 kila siku huku kiwanda cha kutengeneza vifaa vya usafi kinazalisha vipande 4,500 vya vifaa vya usafi kila siku.

Li amesema, "Viwanda hivyo vitatu vina wafanyakazi zaidi ya 3,000, asilimia 95 kati yao ni raia wa Kenya, na wanawawezesha maisha kwa watu zaidi ya 50,000 kwa njia isiyo ya moja kwa moja."

Richard Okello, mwenye umri wa miaka 35, msimamizi katika kiwanda hicho cha kauri cha KEDA, amesema kutumia teknolojia kutoka China kutengeneza vigae bora vya sakafu kumeendeleza ajenda ya Kenya ya makazi ya bei nafuu, kuwapa ujuzi vijana wenyeji na kutoa fursa za ajira.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha