

Lugha Nyingine
Hunter Biden akutwa na hatia katika mashtaka matatu ya uhalifu
![]() |
Hunter Biden akionekana kwenye Ikulu ya Marekani, White House Mei 20, 2024. (Picha na Aaron Schwartz/Xinhua) |
WASHINGTON – Jopo la majaji 12 katika Jimbo la Delaware nchini Marekani siku ya Jumanne limemkuta Hunter Biden, mtoto wa Rais wa Marekani Joe Biden, na hatia ya mashtaka matatu ya kuvunja sheria ya serikali kuu ya Marekani ya kumiliki bunduki, ikiwa ni mara ya kwanza kwa mtoto wa rais aliyeko madarakani kukutwa na hatia ya uhalifu.
Mashtaka hayo ya uhalifu yalimshutumu Hunter Biden mwenye umri wa miaka 54 kwa kusema uwongo kuhusu matumizi yake ya dawa za kulevya alipokuwa akinunua bunduki Mwaka 2018 na hatimaye kumiliki silaha hiyo kinyume cha sheria kwa siku 11. Aliweka alama ya "hapana" kwenye fomu ya ununuzi ya bunduki ya serikali kuu ya Marekani kuhusu matumizi yake haramu ya dawa za kulevya au uraibu wa mihadarati.
Katika majumuisho ya hoja zao za mwisho Jumatatu, waendesha mashtaka hao wamedai kuwa mtoto huyo wa rais alikuwa akitumia dawa za kulevya kwa miaka mingi kabla ya kununua bunduki hiyo na kwamba matumizi hayo ya dawa za kulevya yaliendelea "kwa miezi kadhaa baadaye," kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Utangazaji la CNN.
Timu ya wanasheria ya Hunter Biden, wakati huo huo, imesisitiza kwamba hakukuwa na mashahidi wa matumizi halisi ya dawa za kulevya wakati wa mwezi aliponunua bunduki hiyo.
Hunter Biden anaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka 25 jela na kutozwa faini ya hadi dola 750,000 za Marekani, ingawa si kawaida kwa wakosaji wa mara ya kwanza kupata adhabu hiyo ya juu zaidi.
Rais Biden alisema katika mahojiano ya hivi karibuni kwamba hatamsamehe mtoto wake Hunter kama atakutwa na hatia ya mashtaka ya uhalifu.
Kuhukumiwa na adhabu itakayowezekana ya kufungwa gerezani kwa Hunter Biden kunaongeza zaidi hatari za kisiasa kwa rais huyo katika miezi kabla ya uchaguzi mkuu wa Novemba. Changamoto pana za kisheria za Hunter Biden zimewapa wanasiasa wa Chama cha Republican fursa ya kuonyesha familia ya Biden kuwa ya kifisadi, licha ya kutoweza kuthibitisha makosa yoyote kwa upande wa rais.
Kuongeza tatizo lingine, Hunter Biden anatazamiwa kukabiliana na kesi nyingine kuhusu madai ya kodi huko Los Angeles, California Mwezi Septemba, ambayo inaweza kufichua zaidi habari zisizo za kufurahisha kuhusu familia ya rais huyo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma