Waandamanaji kote Ufaransa waandamana kupinga siasa kali za mrengo wa kulia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 17, 2024
Waandamanaji kote Ufaransa waandamana kupinga siasa kali za mrengo wa kulia
Watu wakishiriki katika maandamano dhidi ya siasa kali za mrengo wa kulia, huko Lille, Kaskazini mwa Ufaransa, Juni 15, 2024. (Picha na Sebastien Courdji/Xinhua)

PARIS - Watu jumla ya 250,000 wameingia mitaani kote nchini Ufaransa siku ya Jumamosi, ikiwa ni pamoja na watu 75,000 jijini Paris, kuandamana dhidi ya siasa kali za mrengo wa kulia, kwa mujibu wa polisi huku Shirikisho Kuu la Wafanyakazi la Ufaransa (CCG) limesema watu 640,000 wamejiunga kwenye mikusanyiko 150 kote nchini humo, ikiwa ni pamoja na watu 250,000 jijini Paris.

Watu tisa wamekamatwa wakiwa wanaandamana jijini Paris, na maofisa watatu wa polisi wamejeruhiwa kidogo, kwa mujibu wa taarifa ya polisi.

Mkuu anayemaliza muda wake wa kundi la La France Insoumise (LFI) katika Bunge la Kitaifa la Ufaransa, Mathilde Panot ametoa wito kwa wapiga kura kuhamasishwa katika uchaguzi wa wabunge, kwenye maandamano hayo ya Paris.

"Wananchi wenzetu watafanya chaguo lao Juni 30 na Julai 7 kwa kupiga kura zao ambalo litakuwa kama ni mrengo mkali wa kulia, au ni sisi," amesema.

Rais wa zamani wa Ufaransa Francois Hollande amesema kuwa atagombea katika uchaguzi wa wabunge kama mgombea huko Correze.

"Ikiwa nimechukua uamuzi huu, ni kwa sababu nimehisi kuwa hali imekuwa mbaya, zaidi kuliko ilivyowahi kuwa .... mrengo mkali haujawahi kuwa karibu sana na mamlaka tangu Ukombozi," amewaambia waandishi wa habari huko Tulle.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alitangaza Jumapili iliyopita kulivunja Bunge, kufuatia kushindwa kwa chama chake katika uchaguzi wa Bunge la Ulaya 2024. Chama cha Renaissance cha Macron kilipata asilimia 14.6 ya kura zote halali zilizopigwa katika uchaguzi wa Bunge la Ulaya 2024, nyuma sana ya chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha National Rally ambacho kilipata asilimia 31.37.

Kwa mujibu wa kura ya maoni mpya kabla ya uchaguzi wa wabunge Juni 30 na Julai 7, chama cha Renaissance kinachoongozwa na rais Macron kinaweza kupata asilimia 18 tu ya kura zote halali katika duru ya kwanza, nyuma ya chama cha Popular Front, asilimia 28.5 na chama cha National Rally ambacho kinaweza kupata asilimia 29.5 ya kura zote.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha