Waandishi wa habari kutoka nchi 16 watembelea Mkoa wa Xinjiang wa China (3)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 25, 2024
Waandishi wa habari kutoka nchi 16 watembelea Mkoa wa Xinjiang wa China
Waandishi wa habari wa nchi za nje wakitembelea Kituo cha Ushirikiano wa Kimataifa cha Mpakani cha China-Kazakhstan cha Horgos Mkoa unaojiendesha wa Xinjiang, Kaskazini-Magharibi mwa China, Juni 16, 2024. (Xinhua/Gu Yu)

URUMQI - Waandishi wa habari kutoka nchi 16 wamehitimisha ziara yao katika Mkoa wa Xinjiang, Kaskazini Magharibi mwa China siku ya Jumapili iliyoanza Juni 15 na kuwapeleka katika mji mkuu wa mkoa huo wa Urumqi, Eneo linalojiendesha la Kabila la Wakazak la Ili na Eneo la Aksu, ambako walipata uelewa wa ana kwa ana kuhusu maendeleo ya mkoa huo na hali ya kulinda utamaduni wa mkoa huo.

Waandishi hao wa habari wamesema wamefurahishwa na utulivu wa kijamii, ukuaji thabiti wa uchumi na utamaduni unaolindwa vyema wa Xinjiang, hali ambayo inapingana na taswira hasi ya Xinjiang ambayo imekuwa ikienezwa na baadhi ya vyombo vya habari vya Magharibi.

"Majengo ya maghorofa, mitaa yenye shughuli nyingi na msongamano wa magari katika miji ya Xinjiang vimenivutia sana," amesema Mustafina Almira, mhariri mkuu wa gazeti la Angren Truth kutoka Uzbekistan.

"Maendeleo hapa ni ya haraka sana ... na kila mtu anafanya kazi kwa bidii ili kujenga maisha bora," amesema Almira, ambaye aliweza kuona bidhaa kutoka mji anakotoka nchini kwake kwenye maduka makubwa katika Mji wa Horgos kwenye mpaka wa China na Kazakhstan.

"Katika miaka ya hivi karibuni, biashara kati yetu imekuwa karibu zaidi kupitia treni za mizigo za China na Ulaya na njia nyinginezo, na nadhani uchumi wa Xinjiang una mustakabali mzuri," amesema Levaz Didberashvili kutoka Georgia, ambaye anafanya kazi katika kituo cha televisheni cha Rustavi 2.

Pamba ya Xinjiang ni jambo linalofuatiliwa sana na vyombo vingi vya habari vya kimataifa. Wakiwa Aksu, waandishi wa habari walitembelea nyumba za wakulima wa pamba na mistari ya uzalishaji wa kampuni za nguo.

"Katika nchi za Magharibi, kile ambacho tumekuwa tukisoma kuhusu ni kile kinachoitwa kulazimisha kufanya kazi na kukandamizwa kwa utamaduni wa Kabila la Wauygur. Tunachokiona hapa ni tofauti kabisa," amesema Nathalie Benelli kutoka Uswisi, mwanzilishi wa chombo cha habari cha kujitegemea, "neue presse."

Ziara hiyo ya siku tisa pia iliwafikisha waandishi wa habari katika maeneo ya kidini yakiwemo Taasisi ya Kiislamu ya Xinjiang huko Urumqi, Msikiti wa Shaanxi katika mji wa Yining, na mapango ya Kizil huko Aksu, ambako walizungumza na watu wa dini na waumini.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha