Mapato yatokanayo na utalii ya Misri yafikia dola bilioni 6.6 katika nusu ya kwanza ya mwaka huu (3)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 03, 2024
Mapato yatokanayo na utalii ya Misri yafikia dola bilioni 6.6 katika nusu ya kwanza ya mwaka huu
Mtalii akitembelea Jumba la Makumbusho ya Taifa ya Ustaarabu wa Misri mjini Cairo, Misri, tarehe 2 Julai 2024. (Xinhua/Ahmed Gomaa)

CAIRO - Misri imetangaza kuwa mapato yake yatokanayo na sekta ya utalii yamefikia dola za Kimarekani bilioni 6.6 katika nusu ya kwanza ya Mwaka 2024, yakipita dola bilioni 6.3 katika kipindi kama hicho Mwaka 2023 ambapo katika taarifa yake siku ya Jumatatu, Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale ya Misri imesema idadi ya watalii waliofika katika nusu ya kwanza ya Mwaka huu ilifikia watu milioni 7.069 kwa rekodi ya juu katika historia.

Idadi ya usiku wenye watalii nchini humo imefikia milioni 70.2 kati ya Januari na Juni, ikizidi rekodi ya mwaka jana ya milioni 67.6 katika kipindi kama hicho.

Kama sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuimarisha utalii, Misri inafanya juhudi kubwa ya kuongeza upatikanaji wa ndege zinazoleta wasafiri kuingia nchini humo na vyumba vya hoteli nchini kote, ikilenga kuhudumia watalii milioni 30 ifikapo Mwaka 2028.

Misri ilipokea idadi inayovunja rekodi ya watalii milioni 14.9 Mwaka 2023. Sekta ya utalii ni mojawapo ya vyanzo vikuu vya fedha za kigeni kwa Misri, ikichangia takriban asilimia 12 katika Pato la Taifa na kutoa ajira kwa watu karibu milioni tatu.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha