Raia wa Japan waandamana kupinga serikali kukaa kimya juu ya unyanyasaji wa kingono katika kituo cha kijeshi cha Marekani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 04, 2024
Raia wa Japan waandamana kupinga serikali kukaa kimya juu ya unyanyasaji wa kingono katika kituo cha kijeshi cha Marekani
Raia wa Japan wakiwa wameandamana mbele ya Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo kupinga serikali ya Japan kuuficha umma kesi zinazodaiwa kuwa za unyanyasaji wa kingono zinazohusisha wanajeshi wa Marekani nchini Japan mjini Tokyo, Japan, Julai 2, 2024. (Xinhua/Zhang Xiaoyu)

TOKYO - Mamia ya raia wa Japan wameandamana mjini Tokyo kupinga vikali serikali ya Japan kuuficha umma kesi za unyanyasaji wa kingono zinazohusisha wanajeshi wa Marekani walioko nchini Japan.

Waandamanaji zaidi ya 350 walikusanyika mbele ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Japan kuonyesha hasira zao siku ya Jumanne jioni, wakiwa wamebeba mabango na vipeperushi vyenye maandishi ya "Nyamazisha Kilio cha Wasichana wa Okinawan," "Rejesha Hadhi kwa Wanawake wa Okinawa," na "Serikali isificha tena Uhalifu wa Wanajeshi wa Marekani."

Vyombo vya habari vya Japan viliripoti kuwa, askari wa kikosi cha majini wa Marekani mwenye umri wa miaka 21 katika Mkoa wa Okinawa, kusini mwa Japan amefunguliwa mashtaka ya kufanya ngono bila ridhaa na kusababisha jeraha mwezi Mei, kufuatia kufunguliwa mashitaka kwa mwanajeshi wa anga wa Marekani kwa madai ya utekaji nyara na unyanyasaji wa kingono wa msichana chini ya miaka 16 mwezi wa Desemba mwaka jana.

Serikali ya Japan, hata hivyo, haikuweka wazi kesi hizo hadi vyombo vya habari vya Japan vilipoziweka wazi mwishoni mwa Juni, na hivyo kuzua hasira kubwa nchini kote.

"Serikali ya Japan, hasa Wizara ya Mambo ya Nje, ilijua lakini iliamua kukaa kimya. Hii siyo demokrasia. Inawapuuza watu wa Japan, wanawake wa Japan, na watu wa Okinawa," amelaani Mizuho Fukushima, mkuu wa chama cha upinzani cha Social Democratic, katika hotuba yake kwenye maandamano hayo.

"Huku ikidai kuwalinda waathiriwa, serikali kwa kweli inawalinda wahalifu," amekosoa Suzuyo Takazato, kiongozi wa kikundi cha kiraia cha Okinawa.

Okinawa inachukua asilimia 70 ya kambi zote za kijeshi za Marekani nchini Japan huku ikichukua asilimia 0.6 pekee ya ardhi ya nchi hiyo. Uhalifu unaofanywa na wanajeshi na wafanyakazi wasiokuwa wa kijeshi wa Marekani umekuwa chanzo cha malalamiko mara kwa mara kwa wenyeji.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha