Bidhaa za China zatoa fursa mpya za biashara kwenye maonyesho ya biashara ya Tanzania

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 09, 2024
Bidhaa za China zatoa fursa mpya za biashara kwenye maonyesho ya biashara ya Tanzania
Viatu na mikoba ya ngozi iliyotengenezwa nchini China ikionyeshwa kwenye Maonyesho ya Kimataifa ya 48 ya Biashara ya Dar Es Salaam (DITF), Tanzania, Julai 6, 2024. (Picha na Emmanuel Herman/Xinhua)

DAR ES SALAAM - Mussa Kaisi, mkulima wa korosho kutoka Mkoa wa Mtwara nchini Tanzania, alitazama trekta lenye nguvu ya HP50 linaloonyeshwa na Kampuni ya Mashine za Kilimo ya Bada (Shandong) ya China kwenye Maonyesho ya Kimataifa ya 48 ya Biashara ya Dar Es Salaam (DITF) jijini Dar es Salaam, Tanzania.

“Nilinunua trekta la aina hii kutoka kwa kampuni hii Machi mwaka huu, na linanisaidia katika kilimo changu cha korosho,” amesema Kaisi ambaye anamiliki hekta 125 za miti ya korosho. Kwa kutumia trekta hilo, anatarajia kuongeza uzalishaji wake wa korosho kutoka tani 20 hadi tani zaidi ya 35 katika msimu ujao wa mavuno, kuanzia Septemba 2024.

“Bidhaa zinazoonyeshwa na kampuni za China zinasaidia wajasiriamali wa Tanzania kuboresha uzalishaji katika sekta mbalimbali zikiwemo za kilimo na viwanda,” ameongeza.

Watanzania wengine wengi wanaotembelea DITF, kama Kaisi, pia wanavutiwa na bidhaa mbalimbali za China zinazoonyeshwa kwenye banda la China. Maonyesho hayo ya biashara, yaliyoanza Juni 28 na yataendelea hadi Julai 13, yanahusisha kampuni zinazoonesha bidhaa zaidi ya 4,000 kutoka nchi 26, zikiwemo kampuni zaidi ya 200 za China.

Yakiwa na kaulimbiu ya "Tanzania: Eneo Lako Bora la Biashara na Uwekezaji," maonyesho hayo ya kibiashara ni shughuli ya kila mwaka inayoonyesha bidhaa za Tanzania na zile kutoka nchi nyingine za Afrika.

Banda la China linaratibiwa na Kampuni ya Kituo cha Biashara na Usafirishaji Bidhaa cha Afrika Mashariki (EACLC), ambayo ni kampuni ya China inayoendeleza biashara kati ya Tanzania na China. EACLC imekuwa ikiandaa maonyesho kwa kampuni za China kwenye maonyesho hayo kwa miaka minne mfululizo.

Cathy Wang, mkurugenzi mkuu wa EACLC Limited, ameelezea matumaini yake kwamba wafanyabiashara wa China wanaoshiriki kwenye maonyesho hayo watapata masoko nchini Tanzania, kugundua vyanzo vya ubora wa juu vya Tanzania, kukamata fursa za uwekezaji na kupata mafanikio.

Banda la China linaonyesha bidhaa kuanzia mashine za kilimo, uzalishaji, usindikaji na uuzaji wa chakula, mashine na vifaa vya umeme, malisho na dawa za mifugo, dawa za mimea na viwanda vya magari.

Waziri wa Viwanda na Biashara wa Tanzania Selemani Jafo amelipongeza banda la China kwenye maonyeho hayo yanayoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania kwa kuonyesha maendeleo ya miundombinu, matarajio ya uwekezaji na maendeleo ya teknolojia.

Ametoa wito kwa wafanyabiashara na kampuni za Tanzania kujifunza kutoka kwenye teknolojia ya kisasa ya China ili kuongeza uzalishaji na kupata mikataba ya kibiashara yenye faida.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha