

Lugha Nyingine
Mwakilishi Maalum wa Rais Xi aipongeza Ufaransa kwa kuandaa kwa mafanikio Michezo ya Olimpiki ya Paris (3)
![]() |
Mwakilishi Maalum wa Rais Xi Jinping wa China na Mjumbe wa Taifa wa China, Shen Yiqin akikutana na Ujumbe wa Olimpiki wa China wakati wa kuwepo kwake mjini Paris, Ufaransa, Agosti 10, 2024. (Xinhua/Peng Ziyang) |
PARIS - Mwakilishi Maalum wa Rais Xi Jinping wa China na Mjumbe wa Taifa wa China, Shen Yiqin siku ya Jumapili alihudhuria hafla ya kufungwa kwa Michezo ya 33 ya Olimpiki mjini Paris na kuipongeza Ufaransa kwa kuandaa kwa mafanikio Michezo ya Olimpiki wakati alipokutana na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na mkewe Brigitte Macron kabla ya kuanza kwa hafla hiyo.
Kwenye mkutano huo, Shen aliwasilisha salamu kutoka kwa Rais Xi na mkewe Peng Liyuan kwa Rais Macron na mkewe na kuishukuru Ufaransa kwa uungaji mkono wake kwa ujumbe wa Olimpiki wa China.
Rais Macron na mkewe wamemwomba Shen kufikisha salamu zao za dhati kwa Rais Xi na mkewe, wamepongeza wanamichezo wa China kwa mafanikio yao mazuri na kuishukuru serikali ya China kwa uungaji mkono wake kwa Ufaransa kuwa mwenyeji wa Michezo ya Olimpiki.
Kwenye mkutano wake na mwenyekiti wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) Thomas Bach Jumamosi, Shen amesema China inapenda kuzidisha ushirikiano wake wa ngazi ya juu wa kirafiki na IOC na itashirikiana na IOC kutoa mchango mpya na mkubwa zaidi katika kuendeleza maendeleo ya Harakati za Olimpiki na kujenga jumuiya yenye mustakabali wa pamoja wa binadamu.
Huku akipongeza ujumbe wa Olimpiki wa China kwa mafanikio yao makubwa katika Michezo ya Olimpiki ya Paris, Bach pia ameishukuru serikali ya China kwa uungaji mkono wake thabiti kwa mambo ya Olimpiki.
“IOC inatarajia kuendelea na ushirikiano wake wa karibu na China na kutuma ishara chanya katika kuunga mkono ushirikiano wa pande nyingi”, ameongeza.
Pande hizo mbili pia zimekubaliana kupinga kuingiza mambo ya kisiasa kwenye michezo.
Wakati wa kuwepo kwake Paris, Shen alitembelea ujumbe wa Olimpiki wa China na kutoa salamu na pongezi kutoka kwa Rais Xi, Kamati Kuu ya CPC na Baraza la Serikali la China.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma