Wanasayansi wa kilimo wa China washinda Tuzo ya Mafanikio ya FAO

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 17, 2024
Wanasayansi wa kilimo wa China washinda Tuzo ya Mafanikio ya FAO
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Qu Dongyu (kulia) akikabidhi Tuzo ya Mafanikio ya FAO kwa Taasisi ya Ulinzi wa Mimea ya Akademia ya Sayansi ya Kilimo ya China (IPPCAAS) katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Chakula Duniani mjini Roma, Italia, tarehe 16 Oktoba 2024. (Xinhua/Li Jing)

ROMA - Taasisi ya Ulinzi wa Mimea ya Akademia ya Sayansi ya Kilimo ya China (IPPCAAS) imetunukiwa Tuzo ya Mafanikio ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) siku ya Jumatano katika hafla iliyoandaliwa na FAO kuadhimisha Siku ya 44 ya Chakula Duniani mjini Roma, Italia.

Mkurugenzi Mkuu wa FAO Qu Dongyu amekabidhi Tuzo ya Mafanikio ya FAO kwa IPPCAAS na kuelezea kazi yake katika kupambana na Viwavijeshi wa Kudondoka kuwa na mchango mkubwa nchini China, kote Asia, na kimataifa, na kupiga hatua kubwa katika kulinda mazao na kupata chakula.

Siku ya Chakula Duniani mwaka huu, ikiwa na kaulimbiu ya "Haki ya vyakula kwa maisha bora na mustakabali bora," inalenga kuongeza uelewa wa kimataifa kuhusu haki ya chakula na kuhamasisha kuifanyia mageuzi mifumo ya kilimo ili kuunga mkono wote wanaishi kwa amani, himilivu, na jumuishi.

Kwa mujibu wa FAO, watu karibu milioni 730 kwa sasa wanakabiliwa na njaa, na watu zaidi ya bilioni 2.8 hawawezi kumudu lishe bora. Hii ina maana kwamba hata kama ulaji wao wa kalori unatosha, wanaweza kuwa hawapokei virutubisho muhimu na aina mbalimbali za lishe ili kudumisha afya njema.

Katika hotuba yake, Qu ametoa wito wa "Kuweka dhamira upya ili kujenga mifumo yenye ufanisi, jumuishi, himilivu, na endelevu zaidi ya kilimo ambayo inaweza kulisha dunia," akisema, "Hakuna muda wa kupoteza; lazima tuchukue hatua za haraka."

Katika ujumbe wake kwa njia ya video, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuwa Dunia bila njaa inawezekana, lakini "mifumo ya chakula inahitaji mageuzi makubwa," ili kuwa na ufanisi, ujumuishi, uhimilivu na uendelevu zaidi.

Kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani, shughuli ya Baraza la Chakula Duniani inafanyika kwenye makao makuu ya FAO kuanzia Oktoba 14 hadi 18.

Tuzo ya Mafanikio ya FAO hutolewa kila baada ya miaka miwili ili kuheshimu taasisi au mtu binafsi kwa ushirikiano bora wa kiufundi au kazi ya kibinadamu katika nyanja za kilimo endelevu, maendeleo ya vijijini, au usalama wa chakula katika ngazi ya nchi.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Renato Lu)

Picha