

Lugha Nyingine
Kundi la BAAS laandamana dhidi ya vikwazo vilivyowekwa na Marekani (2)
![]() |
Watu wakiandamana kupinga vikwazo vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Zimbabwe mbele ya Ubalozi wa Marekani mjini Harare, Zimbabwe, Oktoba 25, 2024. (Xinhua/Tafara Mugwara) |
HARARE - Jumuiya Pana Dhidi ya Vikwazo vya Marekani (BAAS) la Zimbabwe, Ijumaa liliapa kuendelea kupiga kambi mbele ya Ubalozi wa Marekani mjini Harare, mji mkuu wa Zimbabwe, hadi vikwazo vilivyowekwa zaidi ya miongo miwili iliyopita vitakapoondolewa bila masharti.
"Tumekuwa hapa kwa siku 2,036, ambayo ina maana kwamba tumepiga kambi hapa kwa miaka mitano na miezi sita. Tunachotaka ni Marekani kuondoa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Zimbabwe," Makamu Mwenyekiti wa BAAS, Rachael Kamangira amesema kwenye maandamano ya kupinga vikwazo yaliyofanyika mbele ya ubalozi wa Marekani kuadhimisha Siku ya Kupinga Vikwazo ambayo huadhimishwa Oktoba 25 kila mwaka.
Siku ya Kupinga Vikwazo ilianzishwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Mwaka 2019 kupinga hatua ya Marekani na washirika wake wa Magharibi kuiwekewa vikwazo Zimbabwe. Mwezi Machi 2019, BAAS iliweka kambi karibu na eneo la ubalozi wa Marekani.
BAAS itaondoka tu katika eneo hilo kama vikwazo vyote, ambavyo vimeleta kiasi kikubwa cha changamoto kwa Wazimbabwe wa kawaida, vitaondolewa bila masharti, amesema Kamangira.
“Hii ni kambi ya kudumu hata mboga zetu za majani tunalima hapa, kwa sasa tunakaa kwenye mahema, lakini tunafikiria kujenga majengo ya kudumu ili wajue tupo hapa kudumu,” amesema.
Calvern Chitsunge, mwanzilishi mwenza na mwenyekiti wa BAAS, amesema vikwazo hivyo vinadumaza maendeleo ya Zimbabwe, hali ambayo inatatiza maendeleo ya kikanda.
Mwezi Machi, Rais wa Marekani Joe Biden alitia saini amri ya kiutendaji ya kuondoa mpango wa vikwazo vya Zimbabwe uliokuwa umewekwa tangu Mwaka 2003, lakini mara moja akaweka vikwazo kwa watu 11, akiwemo Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa na Makamu wa Rais Constantino Chiwenga kwa madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu na rushwa chini ya Sheria ya Uwajibikaji wa Haki za Kibinadamu ya Magnitsky ya Marekani.
Marekani pia ilidumisha vikwazo kupitia Sheria ya Demokrasia na Kufufua Uchumi ya Zimbabwe ya Mwaka 2001, iliyopitishwa na serikali ya Marekani.
Katika hotuba yake kwenye hafla kuu ya Siku ya Kupinga Vikwazo iliyofanyika katika mjini Bulawayo, Rais Mnangagwa, ambaye ni mwenyekiti wa zamu wa SADC, alisema vikwazo hivyo vinakandamiza uchumi wa nchi hiyo, na kudhoofisha haki yake ya kujiamuliwa na kuathiri mafanikio ya matarajio ya maendeleo ya pamoja ya kitaifa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma