Huduma ya kusafirisha chakula kwa wateja yaongezeka kwa kasi Ethiopia (3)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 29, 2024
Huduma ya kusafirisha chakula kwa wateja yaongezeka kwa kasi Ethiopia
Yisak Sisay mwanzilishi mwenza na meneja mkuu wa kampuni ya kusafirisha vifurushi, akiwa amesimama ofisini mjini Adama, Ethiopia, tarehe 11 Oktoba 2024. (Xinhua/Misikir Temesgen)

ADDIS ABABA - Ndani ya jengo refu mjini Adama, mji mkuu wa Jimbo la Oromia nchini Ethiopia, Kalkidan Daniel alikuwa anapokea simu kutoka kwa mteja mmoja hadi mwingine, akiwapa huduma ya kuwapelekea vyakula wanavyopenda kutoka kwenye hoteli na migahawa kote mjini humo.

Daniel anafanya kazi kusafirisha vifurushi kampuni ya kwanza ya mtandaoni ya kutoa huduma ya kusafirisha chakula kwenda kwa wateja katika mji wa Adama, kilomita takriban 100 mashariki mwa mji Addis Ababa.

"Tulikabiliwa na wakati mgumu sana tulipoanzisha biashara hii miaka miwili iliyopita. Wakazi wenyeji hawakuwa na ufahamu wa huduma ya kusafirisha chakula kilichoagizwa mtandaoni kwenda kwa wateja," amesema Daniel, ambaye ni mkuu wa huduma kwa wateja wa kampuni hiyo.

Idadi ya watumiaji wa huduma hiyo imeongezeka tangu wakati huo kwani wengi wanatambua jinsi ilivyo rahisi kupata vyakula wavipendavyo kupitia huduma hiyo.

Kampuni ya Pick Delivery iliyoanzishwa Julai 2022 inafanya kazi ya kiungo kati ya migahawa na wateja, na hujaza oda zilizowekwa kwenye programu yake au kupitia kituo chake cha huduma kwa wateja. Vyakula hivyo hufikishwa kwa wateja na waendesha baiskeli.

"Biashara inakwenda vizuri na inazidi kuwa maarufu," Daniel amesema. "Tunashuhudia ongezeko la idadi ya oda kila siku kupitia programu na simu."

Yisak Sisay, mwanzilishi mwenza na meneja mkuu wa uendeshaji wa Pick Delivery, amesema kampuni hiyo iliiga uzoefu wa kampuni ya kutoa huduma kama hiyo iliyowekezwa na kampuni ya China mjini Addis Ababa.

Huduma ya kusafirisha chakula kwa wateja ni mpya kwa kiasi fulani nchini Ethiopia, nchi ya pili kwa wingi wa watu barani Afrika ikiwa na watu milioni 120. Sehemu ndogo ya wakazi wa Addis Ababa au Adama wanaifahamu huduma hiyo, na kuacha fursa ya soko ikiwa haijatumika ipasavyo katika nchi hiyo.

Sisay amesema kampuni ya Pick Delivery ililazimika kufanya matangazo ya kina kuhusu huduma hiyo baada ya kuzinduliwa, kwani ni aina mpya ya huduma kwa wakazi wa mji huo.

Pick Delivery pia hubeba na kufikisha bidhaa kutoka kwa wafanyabiashara, ambao huuza bidhaa zao mtandaoni kwa wateja wa Adama.

Biashara ya usafirishaji chakula kinachoagizwa mtandaoni barani Afrika, kama ilivyo kwa tasnia nzima ya biashara ya mtandaoni, bado haijaendelea kikamilifu, kutokana na sababu kama vile muunganiko wa intaneti usiotosheleza na mifumo ya malipo, na vizuizi vya ugavi.

Kwa mujibu wa Kamisheni ya Uchumi wa Afrika ya Umoja wa Mataifa, Kenya, Ushelisheli, Namibia na Afrika Kusini ni nchi pekee za Afrika ambazo wanunuzi wa mtandaoni inazidi asilimia 8 ya wakazi wao. Katika nchi nyingine nyingi za Afrika, uwiano ni chini ya asilimia 5.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha