Botswana yapiga kura kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Mwaka 2024

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 31, 2024
Botswana yapiga kura kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Mwaka 2024

GABORONE - Raia wa Botswana Jumatano walikwenda kwenye vituo vya kupigia kura kupiga kura za kuchagua wabunge na madiwani wapya ambapo foleni za wapiga kura zilianza kupangwa katika vituo vingi kote nchini humo kabla ya muda uliopangwa wa kufungua wa saa 12:30 asubuhi kwa saa za huko.

Watu takriban milioni 1.038 wamejiandikisha kupiga kura katika uchaguzi huo mkuu wa 13 baada ya nchi hiyo kujipatia uhuru.

Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi ya nchi hiyo ya kusini mwa Afrika, zoezi hilo la kupiga kura litachagua wabunge 61 wa Bunge la Taifa na madiwani 609 wa serikali za mitaa, huku chama ambacho kitapata ushindi wa viti angalau 31 kwenye bunge hilo la taifa kikitangazwa kuwa mshindi.

Mokgweetsi Masisi, rais aliyeko madarakani sasa wa Botswana na kiongozi wa chama tawala cha Botswana, Democratic Party, alipiga kura katika kijiji cha Moshupa, Wilaya ya Kusini. Mpinzani mkuu wa Masisi, Duma Boko wa chama cha Mwamvuli wa Mabadiliko ya Kidemokrasia, alipiga kura yake mjini Gaborone, mji mkuu wa nchi hiyo.

Wagombea wengine wa rais ni Dumelang Saleshando wa Chama cha Congress cha Botswana na Mephato Reatile wa Botswana Patriotic Front.

Msemaji wa Tume Huru ya Uchaguzi ya Botswana Osupile Maroba amewaambia waandishi wa habari kwenye kituo cha kusimamia uchaguzi mjini Gaborone kwamba vituo vichache vya kupigia kura havikufunguliwa kwa wakati.

"Lakini vituo vingi vya kupigia kura, zaidi asilimia karibu 99 ya vituo 1,800, vilifunguliwa vyema kwa wakati," amesema.

Vituo vya kupigia kura vilikuwa vikitarajiwa kufungwa saa 1 jioni kwa saa za huko baada ya hapo zoezi la kuhesabu kura ilikuwa lianze mara moja, kwa mujibu wa wasimamizi wa uchaguzi huo.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha