Maonyesho ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa yafunguliwa Shanghai, Tanzania ikiwa nchi mgeni wa heshima

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 05, 2024
Maonyesho ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa yafunguliwa Shanghai, Tanzania ikiwa nchi mgeni wa heshima
Picha ikionyesha Kituo cha kitaifa cha Mikutano na Maonyesho cha China (Shanghai), ukumbi mkuu wa Maonyesho ya 7 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE), Novemba 4, 2024, mjini Shanghai, Mashariki mwa China. (People’s Daily Online)

Maonyesho ya 7 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE) yamefunguliwa rasmi leo Jumanne, Novemba 5 mjini Shanghai, Mashariki mwa China huku Tanzania ikiwa nchi mgeni wa heshima wa maonyesho hayo sambamba na nchi za Ufaransa, Malaysia, Nicaragua, Saudi Arabia na Uzbekistan.

Yakiwa ni maonyesho yanayofanyika mwaka huu tangu China kupitia Mkutano wa Kilele wa Mwaka 2024 wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika mwezi Septemba kutangaza kuondoa ushuru kwa bidhaa bora za kilimo kutoka Afrika zinazoingia katika soko lake, maonyesho hayo yamevutia nchi mbalimbali kutoka Afrika pia na yanachukuliwa kama dirisha la Afrika kutumia vema fursa hiyo ya soko kubwa la China.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na waandaaji, nchi za Afrika kama vile Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Ethiopia, Zimbabwe, Nigeria na nyingine nyingi zimetuma ujumbe wa maofisa, wafanyabiashara na wajasiriamali wakiwa wamekuja na bidhaa mbalimbali kutoka Africa zikiwemo za mazao ya kilimo, madini, mavazi, mazao ya msituni kama vile asali na kazi za mikono na mengine mengi.

Taarifa hiyo imeeleza nchi za Afrika za Benin, Burundi, Madagascar, Namibia na Lesotho zinashiriki kwa mara kwanza maonyesho hayo, ikionyesha kuhamasika kwa nchi za Afrika katika kutumia na kufaidika kikamilifu na soko kubwa la China kupitia matokeo hayo ya mkutano wa kilele wa FOCAC.

Akizungumzia hatua ya China kuondoa ushuru huo na nchi za Afrika kuhamasika kwenye maonyesho hayo, mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji la Ghana, Ayammah Samuel ambaye anahudhuria maonyesho hayo amesema, anaona ni hatua muhimu ambayo itaunga mkono nchi za Afrika kwakuwa nchi nyingi ya nchi hizo ni za kilimo zikizalisha mazao hayo ya kilimo kwa wingi.

“Moja ya changamoto kubwa inayoathiri wakulima wetu na nchi za Afrika ni ukosefu wa soko kwa mazao, hivyo kwakuwa kuna fursa ya soko kama hili kubwa na msamaha wa kodi ambao umetolewa (na China) vitakwenda mbali kutuunga mkono” amesema Ayammah, akiongeza kuwa nchi yake huzalisha kwa wingi kakao na korosho na anatarajia kuona mazao hayo yakipata wateja na kuuzwa katika hali iliyoongezwa thamani.

Yakishirikisha nchi, maeneo na mashirika ya kimataifa 132, maonyesho hayo ya mwaka huu yanayofanyika chini ya kaulimbiu ya 'Zama Mpya, Mustakabali wa Pamoja'  yanachukua eneo la maonyesho lenye ukubwa wa mita za mraba 420,000 huku kampuni bora duniani 209 kati ya 500 zikiwa zimejipanga kushiriki.

Maonyesho hayo yamepangwa kuendelea hadi Nobemba 10 yakiwa na shughuli mbalimbali za mada mahsusi sambamba na majukwaa, uzinduzi wa bidhaa mpya, ujengaji wa mitandao na ushirikiano wa kibiashara na nyingine nyingi.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha