

Lugha Nyingine
Mkulima wa Kahawa wa Uganda: Tunaporejea nyumbani tumeacha wabia wetu kutuuzia bidhaa zetu kote China (2)
Joseph Nkandu mkulima wa kahawa kutoka Uganda ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Wakulima wa Kahawa la Uganda amesema soko la China na Maonyesho ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE) vimejaa matumaini makubwa na kwamba wanaporejea nyumbani wameacha mtandao wa wabia kuendelea kuuza bidhaa zao kote China.
Akizungumza kwenye banda la shirika hilo la maonyesho ya 7 ya CIIE, Nkandu amesema kwamba kwa sasa wanapenya kwenye soko la China, ambalo ameeleza limekuwa likikua kwa kasi na kwamba linakua katika namna ambayo vijana wadogo, kwa mujibu wa takwimu walizoziona za mwenendo wa watembeleaji kwenye banda lao, ndiyo wanaongoza kuulizia kahawa.
“Kwa sasa tunapenya kwenye soko la China. Soko la China ni lenye kuvutia, soko la kahawa linakua kwa kasi China. Linakua katika namna ambayo vijana wadogo, kwa mujibu wa takwimu ambazo tumekuwa tukizifuatilia tangu tuanze maonyesho haya ndiyo wanaoongoza” amesema Nkandu.
Ameongeza kuwa wengi wa vijana hao wanaotembelea banda lake na kununua au kuulizia kahawa ni wenye umri wa miaka kati ya 18 na 30 hivyo kulifanya soko la kahawa la China la siku za baadaye kuwa la kuvutia na lenye kujaa matumaini makubwa.
Nkandu amesema, jambo ambalo ni la muhimu zaidi ni ushirikiano kati ya serikali ya China na zile za nchi za Afrika, na kwa kipekee nchi yake ya Uganda ambao umewezesha wakulima kupokea msamaha wa kodi, hivyo kuweza kuuza aina yoyote ya kahawa kwenye soko la China bila kutakiwa kulipa kodi yoyote.
“Hili ni la kufurahisha sana kwa sababu, sisi wakulima tunaongeza mapato yetu, tunapata uwezo wa kununua bidhaa ambayo pia inatupa uwezo kununua bidhaa zaidi kutoka China kwenda Uganda. Hivyo ni yenye manufaa kwa pande zote pia. Hongera sana kwa Serikali ya China” amesema.
Nkunda amesema, aina mbalimbali za kahawa walizozileta kwenye maonyesho hayo zimependwa sana na wateja Wachina kwasababu zinatoka moja kwa moja kwa wakulima hadi kwa wanunuzi, ni kahawa freshi.
Aidha, wanapomaliza maonyesho hayo ya CIIE, shirika lao limepata wabia Wachina ambao sasa watakuwa na kazi ya kusambaza na kuuza kahawa kote nchini China wakati wao wanaporudi nyumbani Uganda.
Maonyesho ya 7 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE) yaliyoanza Novemba 5 mjini Shanghai, yamefikia tamati jana Jumapili, Novemba 10.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma