Zimbabwe yatarajia kupanua mauzo ya nje nchini China huku kukiwa na kuimarishwa kwa uhusiano wa kibiashara

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 18, 2024
Zimbabwe yatarajia kupanua mauzo ya nje nchini China huku kukiwa na kuimarishwa kwa uhusiano wa kibiashara
Muonyeshaji bidhaa akipiga picha ndani ya banda la Zimbabwe kwenye Maonyesho ya 7 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE) mjini Shanghai, Mashariki mwa China, Novemba 7, 2024. (Xinhua/Zhang Jiansong)

HARARE - Zimbabwe inalenga kuwa na aina mbalimbali za mauzo yake ya nje nchini China huku thamani ya biashara kati ya nchi hizo mbili ikiendelea kukua, Similo Nkala, mkurugenzi wa uendeshaji katika ZimTrade, shirika la kuendeleza biashara la Zimbabwe amesema mwishoni mwa wiki.

"Kwa sasa, mauzo yetu ya nje ya mazao ya matunda na maua yanalenga zaidi masoko katika Umoja wa Ulaya na Uingereza. Sasa tunatazamia kuyafanya kuwa ya anuai, hasa tukilenga kuuza nje matunda na mboga mboga katika soko la Mashariki ya Kati na Asia, ikiwemo China, Malaysia na Indonesia," amesema Nkala.

Hatua muhimu katika uhusiano wa kibiashara kati ya Zimbabwe na China ilifikiwa Mwaka 2022 wakati nchi hizo mbili zilipotia saini makubaliano ya biashara ya machungwa, yakiruhusu kampuni za Zimbabwe kuuza machungwa freshi China.

"Pia hivi karibuni tumetia saini mkataba wa kuuza nje parachichi, ambayo ni hatua kubwa kuelekea kuyafanya mauzo yetu ya nje kuwa ya aina mbalimbali," Nkala ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua.

"Majadiliano yanaendelea kwa ajili yamikataba nyingineya kibiashara, ikiwa ni pamoja na zile za bluuberi, ufuta na pilipili." Ameongeza.

Biashara ya pande mbili kati ya Zimbabwe na China imeongezeka katika miaka ya hivi karibuni, ikionyesha kuimarika kwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Kwa mujibu wa Ubalozi wa China nchini Zimbabwe, thamani ya biashara ilikua kwa asilimia 25.6 katika miezi tisa ya kwanza ya 2024, ikifikia dola za Kimarekani bilioni 3. Zimbabwe iliuza bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 2.1 nchini China huku ikiagiza bidhaa zenye thamani ya dola milioni 951, ikileta urari mzuri wa biashara wa dola takriban bilioni 1.

Wazalishaji wa ngozi wa Zimbabwe pia wamepata umaarufu nchini China. Kwenye Maonyesho ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China Mwaka 2024 (CIIE), kampuni za Zimbabwe zilipata oda nyingi, haswa kwa bidhaa za ngozi zinazohitajika sana.

"Nimeshuhudia wakati wa maonyesho hayo ya biashara nchini China kwamba bidhaa zetu za ngozi zinahitajika sana," Nkala amesema.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha