Watu 16 bado hawajajulikana walipo baada ya boti kuzama Kusini Mashariki mwa Misri (4)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 26, 2024
Watu 16 bado hawajajulikana walipo baada ya boti kuzama Kusini Mashariki mwa Misri
Ambulensi zikionekana karibu na eneo ambalo boti imezama katika Bahari Nyekundu, huko Marsa Alam, Jimbo la Bahari Nyekundu, Misri, Novemba 25, 2024. (Xinhua)

CAIRO - Wamisri wanne na raia wa kigeni 12 bado hawajulikani walipo baada ya boti kuzama katika Bahari Nyekundu mapema asubuhi siku ya Jumatatu, Gavana wa Jimbo la Bahari Nyekundu nchini Misri Amr Hanafy amesema, ambapo katika taarifa yake siku hiyo amesema kuwa jumla ya watu 28 wameokolewa na wana hali nzuri ya kiafya huku shughuli za utafutaji na uchunguzi wa tukio hilo zikiendelea

Jimbo la Bahari Nyekundu limetangaza kwenye ukurasa wake rasmi wa Facebook Jumatatu kwamba boti hiyo ya safari imezama kwenye pwani ya kaskazini ya Marsa Alam, mji wa pwani kusini mashariki mwa Misri kwenye Bahari Nyekundu.

Kwa mujibu wa Hanafy, boti hiyo ilikuwa imebeba abiria 44, wakiwemo Wamisri 13 na wengine 31 kutoka nchi 11: Ujerumani, Uingereza, Marekani, Poland, Ubelgiji, Uswizi, Finland, China, Slovakia, Hispania na Ireland.

Mapema siku hiyo ya Jumatatu, Ubalozi wa China nchini Misri ulisema katika taarifa yake kwamba watalii wawili wa China wameokolewa na vyombo vya majini vilivyokuwa vikipita karibu na eneo la tukio. Ubalozi huo umewasiliana na watalii hao wawili ambao wameripotiwa kuwa na hali nzuri ya kiafya.

Boti hiyo ilifanyiwa ukaguzi wake wa mwisho wa usalama wa baharini mnamo mwezi Machi na ilipewa cheti cha uhalali wa mwaka mmoja, amesema Hanafy.

Hakujakuwa na maoni wala dosari za kiufundi kuhusu boti hiyo, amesema Hanafy, akiongeza kuwa sababu ya awali ya ajali imesemekana kuwa ni wimbi kubwa la bahari kuipiga boti hiyo na kusababisha kupinduka.

Mamlaka husika ya Misri imeripoti kwamba boti ya Sea Story, iliondoka kutoka Port Ghalib ya Marsa Alam siku ya Jumapili na ilikuwa imepangwa kuwasili Hurghada Marina siku ya Ijumaa.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha