

Lugha Nyingine
Wiki ya Mitindo ya Katutura ya Namibia yajivunia uvumbuzi na ujumuishaji
![]() |
Wanamitindo wakionyesha mavazi yaliyobuniwa katika Wiki ya Mitindo ya Katutura mjini Windhoek, Namibia, Novemba 23, 2024. (Picha na Ndalimpinga Iita/Xinhua) |
WINDHOEK – Shughuli ya nne ya Wiki ya Mitindo ya Katutura (KFW) imehitimishwa katika mji mkuu wa Namibia, Windhoek, Jumamosi jioni, huku uvumbuzi na ujumuishaji ukifuatiliwa.
Eneo la Katutura, ambalo hapo awali lilikosa jukwaa la kuonyesha vipaji na kutoa fursa kwa wabunifu, limeshuhudia mabadiliko kwa kuzinduliwa kwa KFW mwaka 2019.
Dennis Hendriks, mwanzilishi wa Wiki ya Mitindo ya Katutura, amesema kuwa shughuli hiyo ya siku mbili, iliyofanyika chini ya kaulimbiu ya “Kuvumbua Mitindo Leo,” inasherehekea mafungamano ya mitindo, utamaduni na utalii wa ndani.
"Kwa hivyo maonyesho hayo ni jukwaa jumuishi kwa wabunifu wote wanaoibukia na wabobezi, wanamitindo na wasanii kuonyesha vitu vinavyoangazia uanuwai tajiri ambao unawakilisha mazingira ya mtindo wetu," amesema siku ya Jumapili.
Maonyesho hayo yalivutia washiriki wenyeji na wabunifu wa mitindo kutoka nchi nyingine, zikiwemo Afrika Kusini, Botswana na Angola. Wanamitindo walitembea kwenye jukwaa la kuonyesha ubunifu moja kwa moja, wakionyesha mavazi ya kijadi, ya kisasa na ya kufumwa. Miundo ya mapambo ya vito, ikijumuisha shanga, vikuku na pete, iliongeza mvuto wa maonyesho hayo, wakati mikoba na vifaa vilivyotengenezwa kutokana na vitu vilivyobadilishwa matumizi upya vilikamilisha vipande mbalimbali vya mtindo.
Washiriki wamepongeza jukwaa hilo kwa kutoa fursa kwa wabunifu wenyeji. Naha Neumbo, mbunifu wa mitindo wa nchini humo ambaye amekuwa akionyesha mkusanyiko wake wa mitindo ya mavazi kwa mwaka wa tatu, amesema kuwa KFW imeongeza biashara yake ya mitindo.
Kabla ya shughuli hiyo, Neumbo, mbunifu wa mitindo tangu Mwaka 2011, alikuwa akifanya kazi akiwa nyumbani, akitengeneza mavazi kwa marafiki na jamaa wa karibu. Hata hivyo, onyesho lake la kwanza kwenye KFW liliashiria mabadiliko, likisababisha ongezeko la wateja wake na kupanuka kwa huduma mbalimbali kwa wateja wengi zaidi.
Tangu wakati huo, pia amesanifu mavazi kwa ajili ya shindano rasmi la kitaifa la urembo la nchi hiyo, Miss Namibia. "Kwa kweli ni njia ya uuzaji kwa wabunifu wa mitindo wasiojulikana sana wanaotaka kukua," amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma