Lugha Nyingine
Tamasha la Michezo ya 12 ya Kijadi ya Makabila Madogo ya China lafanyika Sanya
Msanii akifanya onyesho kwenye tamasha la Michezo ya 12 ya Jadi ya Makabila Madogo ya China mjini Sanya, Mkoani Hainan, Kusini mwa China, Novemba 26, 2024. (Xinhua/Yang Wenbin) |
SANYA, China – Tamasha la Michezo ya 12 ya Jadi ya Makabila Madogo ya China limefanyika katika Bustani ya Yasha mjini Sanya, Mkoa wa Hainan, Kusini mwa China, likionyesha uanuwai wa kitamaduni na umoja wa China ambapo tamasha hilo lilianza kwa sherehe ya ukaribisho na maonyesho ya kitamaduni kwenye Eneo la Kivutio la Tianya Haijiao.
Wanamichezo na wageni walifurahia burudani za kuvutia za nyimbo na ngoma za jadi, maonyesho ya maigizo, maonyesho ya desturi za watu, na maonyesho ya urithi wa utamaduni usioshikika wa eneo hilo huku shughuli mbalimbali zikichangamsha zaidi uzoefu wa watu.
Maonyesho hayo ya kitamaduni yalifikia kilele chake wakati washiriki walipopeana zawadi na kukutana pamoja kucheza Ngoma ya Gongtong ya watu wa kabila la Wali, inayotokana na miondoko ya nyimbo za kijadi za watu wa Danzhou.
"Sanya ni mji wa pwani unaojulikana kwa haiba yake ya kipekee ya mambo ya baharini," amesema Wu Yan, mtayarishaji mkuu wa maudhui ya tamasha hilo. "Tumeandaa maonyesho takriban 40 ya maudhui ya makabila katika Eneo la Kivutio la Tianya Haijiao, tukitengeneza 'mandhari yenye maudhui ya makabila' kando ya bahari."
"Kwa kuchanganya mandhari ya pwani, maonyesho ya kitamaduni ya makabila, na vipengele vya mazingira ya asili kama vile misitu, ufukwe na anga ya buluu, tulilenga kuunganisha mambo maalumu ya Mkoa wa Hainan na mila za makabila na mitindo ya kisasa," Wu ameeleza.
Kwenye tamasha kuu, wanamichezo walifurahia maonyesho ya kuvutia na walishiriki kwa shauku katika michezo. Wakati shughuli hiyo ikifikia tamati, hali ya sherehe iliongezeka huku watumbuizaji wakialika wanamichezo kwa hamasa kubwa kuimba na kucheza, ikitengeneza hali ya shangwe iliyodhihirisha moyo wa umoja na urafiki.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma