Wafanyakazi wa kibinadamu wa UN wahamasishwa kutoa msaada nchini Lebanon katika siku ya kwanza ya usimamishaji mapigano

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 28, 2024
Wafanyakazi wa kibinadamu wa UN wahamasishwa kutoa msaada nchini Lebanon katika siku ya kwanza ya usimamishaji mapigano
Picha hii iliyopigwa Novemba 26, 2024 ikionyesha uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya anga ya Israel mjini Bekaa Magharibi, Lebanon. (Picha na Maher Kamar/Xinhua)

UMOJA WA MATAIFA – Usimamishaji mapigano kati ya Israel na Lebanon ni matumaini makubwa zaidi ya kumaliza mateso makubwa katika janga baya zaidi la kibinadamu kuwahi kutokea katika kizazi kimoja, Tom Fletcher, naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kibinadamu na mratibu wa misaada ya dharura, ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii X siku ya Jumatano akiongeza kuwa "wafanyakazi wa kibinadamu wataendelea kuitikia ili kufikia watu wahitaji,"

Huku makubaliano ya kusimamisha mapigano yakianza rasmi mapema Jumatano (kwa saa za huko), wafanyakazi na washirika wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wamehamasishwa kwa makundi kutoa msaada na kuunga mkono watu wahitaji.

Katika siku ya kwanza ya usimaishaji huo wa mapigano, huku kukiwa na joto lililoshuka chini, malori 11 kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) yalipeleka vifaa vya dharura kwa watu zaidi ya 3,000 mjini Baalbek, zikiwemo mablanketi, magodoro, jaketi nzito, vitambaa vya plastiki, taa za kutumia nishati ya jua na majamvi ya kulalia.

"Mara tu baada ya usimamishaji mapigano kuanza kutekelezwa saa 10 alfajiri (Jumatano, kwa saa za huko), wakazi wa kusini mwa Lebanon, vitongoji vya kusini mwa Beirut na (bonde la) Bekaa walianza kurejea baada ya miezi kadhaa ya kulazimika kukimbia makazi yao," imesema UNHCR.

Shirika hilo limesema kuwa wataendelea kufanya kazi kwa karibu na mamlaka za serikali za maeneo husika na washirika ili kutoa msaada wa dharura kwa watu walioathirika ili kuwaweka katika hali ya kupata joto na salama wakati wa majira haya ya baridi.

UNHCR imekabidhi vitu vya misaada zaidi ya 330,000 kwa watu zaidi ya 190,000 nchini Lebanon tangu Septemba 23.

Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) linaendelea kuunga mkono watoto ambao wameathiriwa kwa kiasi kikubwa na mgogoro huo, na kutoa uungaji mkono wa dharura wa kisaikolojia kwa maelfu ya watoto na walezi.

Mgogoro huo kati ya Israel na Hezbollah umeharibu maisha ya watu, huku watu zaidi ya 3,800 wameuawa, wengine 15,800 kujeruhiwa, na karibu 900,000 kulazimika kuwa wakimbizi wa ndani, sambamba na watu zaidi ya nusu milioni waliokimbia makazi yao kuvuka mipaka, mamlaka za Lebanon zimesema.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha