Mabaki ya miili ya askari wahanga 43 wa China katika Vita vya Korea yarudishwa nyumbani kutoka Jamhuri ya Korea

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 29, 2024
Mabaki ya miili ya askari wahanga 43 wa China katika Vita vya Korea yarudishwa nyumbani kutoka Jamhuri ya Korea
Wanajeshi wakisindikiza majeneza yenye mabaki ya askari wahanga 43 wa Jeshi la Kujitolea la Watu wa China (CPV) katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Taoxian huko Shenyang, Mkoa wa Liaoning, kaskazini mashariki mwa China, Novemba 28, 2024. (Picha na Han Qiyang/Xinhua)

SHENYANG - Mabaki ya askari wahanga 43 wa Jeshi la Kujitolea la Watu wa China (CPV) waliofariki kwenye Vita vya Kupinga Mabavu ya Marekani na Kuisaidia Korea (1950-1953) yamerejeshwa China siku ya Alhamisi kutoka Jamhuri ya Korea ambapo majira ya saa 6:07 mchana, Ndege ya Jeshi la Anga la China ya Y-20, iliyobeba mabaki ya miili ya askari hao na vitu vyao vingine 495 ilitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Taoxian huko Shenyang, Mkoa wa Liaoning wa China.

Katika wakati wa kutua kwa ndege hiyo, ilipigwa mizinga ya salamu ya heshima na ya kutoa maji ya kani kubwa, huku askari wakibeba majeneza kutoka kwenye ndege hiyo kabla ya hafla ya kumbukumbu kufanyika kwenye uwanja huo wa ndege.

Watu takriban 1,000, wakiwemo wajumbe kutoka serikali kuu na za mitaa, wanajeshi, askari waliostaafu, na jamaa wa wahanga wa CPV, walihudhuria hafla hiyo.

Kufuatia kuwekwa kwa majeneza yaliyokuwa yamefunikwa kwa Bendera Nyekundu ya Nyota Tano, ambayo ni bendera ya taifa la China, washiriki waliinama mara tatu kwa ukimya wa heshima mbele ya mabaki ya miili ya askari hao. Mabaki hayo yatazikwa katika makaburi ya wahanga huko Shenyang.

Baada ya Jamhuri ya Korea kukabidhi mabaki ya miili ya wahanga na vitu vyao kwa upande wa China huko Incheon Asubuhi ya siku hiyo ya Alhamisi, China ilifanya hafla ya kumbukumbu kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Incheon. Kwenye hafla hiyo, ulipigwa muziki wa wimbo wa taifa wa China, na kila jeneza lilifunikwa kwa bendera ya taifa.

Washiriki wa hafla hiyo waliinama mara tatu kwa heshima ya wahanga hao kabla ya majeneza yao kuwekwa kwenye ndege.

Kuanzia Mwaka 2014 hadi 2023, China na Jamhuri ya Korea zikifuata sheria ya kimataifa na kanuni za ubinadamu, zimekamilisha kwa mafanikio makabidhiano 10 mfululizo ya mabaki ya miili ya askari wahanga 938 wa CPV na vitu vyao husika katika Jamhuri ya Korea. Vita hivyo vya Korea vilianza mwezi Juni 1950, miezi minane tu baada ya kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China. Kutokana na ombi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea (DPRK), vikosi vya ardhini vya China viliingia Peninsula ya Korea mnamo Oktoba 19, 1950. Jumla ya askari milioni 2.9 wa Jeshi la kujitolea la Watu wa China walishiriki kwenye vita hivyo vilivyodumu karibu kwa miaka mitatu, ambapo zaidi ya askari 360,000 waliuawa au kujeruhiwa kwenye vita hivyo.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha