Walebanon waliokimbia makazi wamiminika nyumbani baada ya kusimamisha vita, wakiwa na furaha, hasara na ukosefu wa uhakika

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 29, 2024
Walebanon waliokimbia makazi wamiminika nyumbani baada ya kusimamisha vita, wakiwa na furaha, hasara na ukosefu wa uhakika
Watu waliolazimika kukimbia makazi yao wakiwa njiani kuelekea nyumbani baada ya kusimamisha vita katika vitongoji vya kusini mwa Beirut nchini Lebanon, Novemba 27, 2024. (Str/Xinhua)

BEIRUT – Huku makubaliano ya kusimamisha mapigano kati ya Lebanon na Israel yakiwa yameanza kutekelezwa alfajiri siku ya Jumatano, Jihad Nasrallah, pamoja na maelfu ya Walebanon wengine waliolazimishwa kukimbia makazi yao, hawakuwa na muda wa kupoteza ambapo kabla ya jua kuchomoza siku hiyo, walikusanya kila kilicho chao na kuanza safari iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu kurejea kwenye nyumba zao kusini mwa Lebanon.

Barabara zilikuwa zimejaa watu waliokuwa wakirudi, nyuso zao zikiwa na mchanganyiko wa furaha na huzuni inayowazunguka. Wengi wamestahimili mateso ya mwaka zaidi ya mmoja ya kulazimika kukimbia makazi yao, kurudi kwao kunaashiria furaha ya kurejesha nyumba zao lakini pia huzuni ya kupoteza mavuno, mali zilizoharibiwa, na wapendwa wao waliopoteza maisha yao kwenye vita.

"Waliolazimika kukimbia makazi yao hawakuweza kupata usingizi, wakisubiri kwa hamu kupambazuke," Jihad ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua akiongeza: "Kulikuwa na machozi ya furaha wakati watu wakiagana, na honi za gari zilisikika katika kusherehekea."

Katika kijiji cha kusini-mashariki cha Kfarhamam, watu wengi wanaorejea nyumbani walipoteza makazi yao kutokana na mashambulizi ya mabomu ya Israel. Bado, wanakijiji hao hawakufadhaika, kwani kipaumbele chao, kwa mujibu wa kijana Hassan Abdul Karim, kilikuwa ni kuachana na hali yao ya kulazimishwa kukimbia makazi na kurudi katika maeneo yao ya asili.

"Kulazimishwa kukimbia makazi ni dhuluma, inafedhehesha, na inasumbua sana," Abdul Karim ameliambia Xinhua. "Ni afadhali tuishi katika mahema kwenye magofu ya nyumba zetu kuliko kubaki katika kumbi za shule, tukiwa tumesongamana pamoja na familia nyingine tano hadi nane. Kwa hiyo tumerudi, tukiwa tumebeba magodoro na blanketi kwenye paa za magari yetu."

Jeshi la Lebanon lilikuwa limehamasishwa katika mpambazuko wa kwanza, likipeleka tingatinga na malori kukarabati barabara zilizoharibiwa na mashambulizi ya anga katika Bonde la Bekaa na kusini mwa Lebanon.

Wakati huo huo, askari wa Kikosi cha Usalama wa Ndani walikuwa wakisimamia matumizi ya barabara katika makutano muhimu, wakati timu za matibabu kutoka Shirika la Msalaba Mwekundu na Mamlaka ya Kiislamu ya Afya ya Lebanon zilijiweka kwenye lango la jiji kushughulikia dharura.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha