Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuenea kwa jangwa wafunguliwa Riyadh (3)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 03, 2024
Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuenea kwa jangwa wafunguliwa Riyadh
Picha hii iliyopigwa tarehe 2 Desemba 2024 ikionyesha onyesho kwenye ufunguzi wa Mkutano wa 16 wa Nchi Watiasaini (COP16) kwenye Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Hali ya Kuenea kwa Jangwa (UNCCD) mjini Riyadh, Saudi Arabia. (Xinhua/Wang Dongzhen)

RIYADH - Mkutano wa 16 wa Nchi Watia saini (COP16) kwenye Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Hali ya Kuenea kwa Jangwa (UNCCD) umefunguliwa mjini Riadh, Saudi Arabia Jumatatu, ukitoa wito wa juhudi za dunia nzima kurejesha ardhi na kuimarisha ustahimilivu wa ukame.

Ukiwa umepangwa kufanyika hadi Desemba 13 chini ya kaulimbiu ya "Ardhi Yetu. Mustakabali Wetu wa Siku za Baadaye," mkutano huo una umuhimu mkubwa ukiwa mkutano mkubwa zaidi wa Umoja wa Mataifa unaojikita katika ardhi hadi sasa na mkutano wa kwanza kufanyika katika eneo la Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika.

Akihutubia ufunguzi wa mkutano huo, Ibrahim Thiaw, katibu mtendaji wa UNCCD, amezungumzia umuhimu wa kurejesha ardhi, akisema hatua hiyo ni kama "moja ya zana madhubuti za kushughulikia baadhi ya changamoto kubwa za zama yetu -- mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa usalama wa chakula, ukosefu wa usawa wa kiuchumi, uhamiaji wa kulazimishwa, na hata kukosekana kwa utulivu duniani."

Ifikapo mwaka 2050, watu wapatao bilioni 7.5 watakuwa wakiathiriwa na ukame, katibu mtendaji huyo amesema, akitoa wito wa kuchukua hatua za haraka.

Kwa upande wake Waziri wa Mazingira, Maji na Kilimo wa Saudi Arabia, Abdulrahman Abdulmohsen AlFadley amesema kuwa watu zaidi ya bilioni 3 wanaathiriwa na uharibifu wa ardhi kila mwaka kutokana na kupoteza hekta milioni 100 za ardhi, misitu na mbuga.

"Hii itaongeza viwango vya uhamiaji, utulivu na usalama miongoni mwa jamii nyingi," amesema.

Kwenye mkutano huo wa COP 16 unaoendelea, ambao utaadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwa UNCCD, wajumbe wanatarajiwa kuamua juu ya hatua za pamoja ili kuharakisha juhudi za kurejesha ardhi, kuongeza uwezo wa kustahimili ukame na dhoruba za mchanga, kurejesha rutuba ya udongo, na kuongeza uzalishaji wa chakula rafiki kwa mazingira ya asili ifikapo Mwaka 2030 na baadaye.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha