

Lugha Nyingine
UNESCO yaiorodhesha Sikukuu ya Mwaka Mpya wa Jadi wa China kwenye orodha ya urithi wa utamaduni usioshikika (2)
ASUNCION -Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limeiorodhesha Sikukuu ya Mwaka Mpya wa Jadi wa China, ambayo ni desturi za kijamii za watu wa China katika kusherehekea mwaka mpya wa jadi, kwenye Orodha ya Urithi wa Utamaduni Usioshikika wa Binadamu jana Jumatano.
Uamuzi huo umetolewa kwenye Mkutano wa 19 wa Kamati ya Kati ya Serikali kwa ajili ya Kulinda Urithi wa Utamaduni Usioshikika, unaofanyika nchini Paraguay kuanzia Desemba 2 hadi 7. Kamati imeitambua sikukuu hiyo kwa shughuli mbalimbali za kimila na mambo ya kipekee ya kitamaduni ambayo yanajumuisha jamii zote za Wachina.
UNESCO imesisitiza kuwa Sikukuu ya Mwaka Mpya wa Jadi wa China, ni alama ya kuanza kwa Mwaka Mpya kwa Kalenda ya Kilimo ya China, inahusisha desturi mbalimbali za kijamii, ikiwa ni pamoja na kuomba bahati nzuri na kujumuika kwa wanafamilia. Pia inahusisha shughuli zinzopangwa na wazee na hafla za sherehe za umma zinazoandaliwa na jamii.
Nyaraka za UNESCO zinaonesha kuwa, maarifa na desturi za kijadi kuhusu Sikukuu hiyo hupitishwa kwa njia isiyo rasmi ndani ya familia na jamii, na vilevile kwa njia rasmi kupitia mfumo wa elimu. Ufundi na ujuzi wa kisanii unaohusiana na sikukuu hiyo huenezwa na kusambazwa kwa umma kupitia mafunzo, kuhimiza maadili ya familia, mshikamano wa kijamii, na amani, huku vikitoa hisia ya utambulisho wa kitamaduni.
Kamati hiyo pia imesisitiza kuwa sikukuu hiyo inaonyesha mapatano kati ya binadamu na mazingira ya asili na kusaidia maendeleo endelevu katika maeneo kama vile usalama wa chakula na elimu. Pia ina mchango mkubwa katika kuongeza ufahamu wa ulinzi wa mazingira.
Naibu Waziri wa Utamaduni na Utalii wa China, Rao Quan, ambaye anaongoza ujumbe wa China kwenye mkutano huo wa UNESCO, ameelezea shukrani zake kwa utambuzi huo.
Amesisitiza kuwa Mwaka Mpya wa Jadi wa China ni sikukuu muhimu zaidi ya jadi ya China, inayoonyesha matumaini ya watu wa China ya maisha bora, uhusiano thabiti kati ya familia na nchi, na maadili ya mapatano kati ya binadamu na mazingira ya asili.
Kwa kuorodheshwa kwa sikukuu hiyo kwenye orodha hiyo, China sasa ina mambo 44 ya kitamaduni au desturi yanayotambuliwa na UNESCO kama Urithi wa Utamaduni Usioshikika wa Binadamu.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma